Jan 31, 2024 02:43 UTC
  • Papa adai Maaskofu wa Afrika wanapinga kubarikiwa 'mashoga' kwa sababu ya imani za kiutamaduni

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amesema, upinzani kutoka kwa maaskofu wa kikatoliki barani Afrika kwa agizo lake la kuwaruhusu makasisi kubariki watu wa jinsia moja wanaoishi kiunyumba, ni "kesi maalumu" inayochochewa na imani zao za kiutamaduni.

Papa ametoa maoni hayo wakati wa mahojiano na gazeti la Italia La Stampa akijibu ukosoaji ulioenea dhidi ya idhini yake ya hati ya Vatikani inayoruhusu kuwabariki watu wa jinsia moja wanaoishi kiunyumba.
 
Tamko hilo liitwalo ‘Fiducia Supplicans’, lililochapishwa mwezi uliopita, linafungua uwezekano wa kuwabariki wale waitwao 'wanandoa' ambao uhusiano wao si “halali” katika Kanisa Katoliki, wakiwemo watu wasiofunga ndoa, waliotalikiana na kufunga ndoa tena, na watu wa jinsia moja wanaoishi kiunyumba.
 
Mapema mwezi huu, Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM) - chama cha Maaskofu wa Kikatoliki katika bara hilo - lilishutumu uamuzi huo wa Papa likisema ni "usiofaa".
Kardinali Fridolin Ambongo 

Rais wa SECAM Kardinali Fridolin Ambongo alisema katika taarifa kwamba kuruhusu mila kama hiyo kunaweza kusababisha "mkanganyiko" na "kupingana moja kwa moja" na maadili ya kiutamaduni ya jamii za Kiafrika.

 
Hata hivyo katika mahojiano na La Stampa, Papa Francis amesema, ukiondoa Waafrika ambao ni kesi maalumu, wale wanaopinga uamuzi wake hatimaye watauelewa.
 
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amedai kuwa, uamuzi wa kutoa baraka kwa watu wa jinsia moja wanaoishi kiunyumba haukusudii kuidhinisha maisha yanayoweza kuwa ya dhambi, lakini ni kwa ajili ya watu binafsi wanaotaka kuwa karibu na Mungu.
 
Maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja wanaotambulika kama 'mashoga', yanayohusisha vitendo vichafu vya liwati na usagaji yangali yanatambulika kama uovu na uhalifu katika nchi nyingi za Afrika ikiwa ni pamoja na Uganda, ambako ngono za watu wa jinsia moja zinaweza kupelekea mhusika kuhukumiwa kuanzia kifungo cha hata maisha jela au hata adhabu ya kifo.../
 

Tags