Feb 11, 2024 06:55 UTC
  • Waislamu Marekani: Joe Biden ni mshirika wa jinai za Israel Gaza

Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani (CAIR) limetangaza katika taarifa yake kuwa: Rais Joe Biden wa Marekani si tu kwamba, ni mtazamaji wa jinai za Israel huko Gaza, bali kwa ukimya wake, ametoa idhini ya kuendelea jinai hizo na ni mshirika katika jinai hizo za Israel.

Taarifa ya baraza hilo imeeleza kuwa, ingawa utawala wa Biden umeongeza ukosoaji wake wa maneno kwa vita vya Israel huko Gaza, lakini kiutendaji unaendelea kuunga mkono kwa nguvu utawala huo bandia.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani imekosoa vikali uungaji mkono wa serikali ya Biden kwa utawala haramu wa Israel hasa kisilaha na kilojistiki.

Wananchi wa Marekani wamekuwa wakifanya maandamano makubwa wakipinga uungaji mkono na himaya ya serikali ya Washington kwa jinai na mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutaka kusitishwa mara moja vita huko Palestina.

Maandamano hayo ya wananchi ya kupinga uungaji mkono na misaada ya Washington kwa jinai za Israel, yameshamiri huku hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ikizidi kuwa mbaya kila siku kutokana na kimya cha madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

 

Wakati huo huo, nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa, kumefanyika mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika Marekani ambapo nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Tags