Feb 22, 2024 02:39 UTC
  • Rais wa Brazil afananisha jinai za Israel na zile za Hitler wa Ujerumani

Jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza zinahesabiwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya karibuni na aghalabu ya jinai hizo zimetajwa kuwa ni maangamizi ya kizazi huku zikilinganishwa na uhalifu ulizofanywa na Adolf Hitler, kiongozi Manazi wa Ujerumani, katika Vita vya Pili vya Dunia.

Kuhusiana na sula hilo, Rais Luis Inacio Lula Da Salva wa Brazil ametahadharisha kuwa kinachojiri katika Ukanda wa Gaza dhidi ya wananchi wa Palestiuna hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi kingine chochote cha historia isipokuwa wakati wa Hitler. Rais wa Brazil amesisitiza kuwa, kile kinachotokea Ukanda wa Gaza si vita bali ni mauaji ya kimbari yanayokumbusha matendo ya Hitler. 

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 29,195, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 69,000 wamejeruhiwa katika vita vya Israel na Marekani dhidi ya Gaza. Hospitali nyingi na vituo vya matibabu vimelengwa na kuharibiwa kwa mashambulio ya Israel. Aidha shuhguli za utoaji huduma za kibinadamu na uokoaji kwa majeruhi wa vita zimekwama na hata kusimama kutokana na mashambulizi mtawalia ya Israel ikisaidiwa kwa hali na mali na baadhi ya nchi za Magharibi. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, Israel haiwaruhusu wawakilishi wa shirika hilo kuingia na kuchunguza hali ya Hospitali ya Nasser. Hiyo ni hospitali kubwa zaidi inayopatikana kusini mwa Gaza ambayo haitumiki kufuatia mashambulizi ya Israel. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuhusiana na hali ya Ukanda wa Gaza kwamba: "Hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha adhabu jumuishi dhidi ya watu wa Palestina. Hali ya kibinadamu huko Gaza haiwezi kuelezeka kwa maneno, na hakuna sehemu au mtu aliye salama katika eneo hilo." Jinai za  Israel dhidi ya Wapalestina zimekithiri kiasi kwamba katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na sisitizo la Israel la kuendeleza vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, nchi mbalimbali sambamba na kulaani jinai za Israel zimetoa wito wa kukomeshwa ukatili huo Ukanda wa Gaza. 

Kuhusiana na hilo, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza. Mashtaka ya Afrika Kusini yanaeleza kuwa, Israel imekiuka masharti ya Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Jinai za Mauaji  ya Kimbari. Kufuatia mashtaka hayo, Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliamua kwamba, Israel lazima ichukue hatua zinazohitajika ili kuzuia uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya binadamu. 

Israel yaendeleza mashambulizi dhidi ya Gaza 

Nchi nyingi zimeunga mkono hatua hiyo ya Afrika Kusini na kutaka kukomeshwa uhalifu wa Israel dhidi ya Wapalestina. Tirana Hassan Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Iwapo utawala wa Israel hautazingatia taratibu au amri za mahakama, jamii ya kimataifa lazima ihakikishe kunakuwepo mashinikizo ya kila aina ili kuulazimisha utawala huo utekeleze ipasavyo hatua hizo."   

Kiwango cha jinai za Israel huko Palestina kimewafanya hata washirika wa Ulaya wa utawala huo haramu kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya raia. Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ameeleza katika taarifa yakke akimhutubu Rais Joe Biden wa Marekani bila ya kuitaja nchi hiyo kuwa: "Ikiwa unaamini kuwa watu wengi wanauawa huko Gaza, labda unapaswa kutoa silaha kidogo ili kuzuia kuuliwa watu wengi zaidi. Inashangaza kuona nchi mbalimbali  zinasema mara kwa mara kuwa Israel inaua idadi kubwa ya raia huko Gaza, lakini hazichukui hatua zinazoeleweka kuzuia mauaji hayo." Joe Biden aliwahi kusema katika hotuba yake huko nyuma kwamba jibu la Israel kwa shambulio la Hamas la Oktoba 7 limepindukia mipaka.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa EU 

Matamshi ya hivi sasa ya Rais wa Brazili na kufananisha kwake jinai za Israel huko Gaza na uhalifu uliofanywa na Hitler wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, kwa mara nyingine yameelekeza maoni na fikra za walimwengu kwenye maafa yanayotokea katika ardhi hiyo ndogo yenye idadi kubwa ya watu. Pamoja na haya yote, swali muhimu linalojitokeza ni kwamba, ni hatua zipi zilizochukuliwa na jamii ya kimataifa ili kusitisha maafa hayo ya kutisha? 

Tags