Mar 01, 2024 06:47 UTC
  • Putin aonya juu ya hatari

Rais Vladmir Putin wa Russia ameziambia nchi za Magharibi kuwa, ziko hatarini kuzusha vita vya nyuklia iwapo zitatuma wanajeshi kupigana nchini Ukraine, akionya kwamba Moscow ina silaha za kushambulia maeneo ya Magharibi.

Vita vya Ukraine vimesababisha mzozo mbaya zaidi katika uhusiano wa Moscow na nchi za Magharibi tangu baada ya Mgogoro wa Makombora wa Cuba wa 1962. Putin aliwahi kuzungumzia hatari ya makabiliano ya moja kwa moja kati ya NATO na Russia, lakini onyo lake kuhusu vita vya silaha za nyuklia alilolitoa jana Alhamisi lilikuwa la wazi zaidi.

Akiwahutubia wabunge na shakhsia wengine wa nchi hiyo, Rais Vladimir Putin, aliye na umri wa miaka 71, alikariri shutuma zake kwamba nchi za Magharibi zina nia ya kuidhoofisha Russia, na kusema viongozi wa Magharibi hawaelewi hatari kubwa ya uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya Russia.

Rais Putin ametoa onyo hilo la vita vya nyuklia akiashiria wazo lililotolewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron siku ya Jumatatu iliyopita, la kutaka wanachama wa NATO wa Ulaya kutuma wanajeshi wa nchi kavu nchini Ukraine; pendekezo ambalo lilikataliwa haraka na Marekani, Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibi.

"(Mataifa ya Magharibi) lazima yatambue kwamba sisi pia tuna silaha zinazoweza kulenga shabaha kwenye maeneo yao. Haya yote yanatishia mzozo wa matumizi ya silaha za nyuklia na uharibifu wa ustaarabu. Je, hawatambua hivyo?!", amehoji Rais wa Russia.

Vladimir Putin

Amesema: "Vikosi vya kimkakati vya nyuklia vya Russia viko katika hali ya utayarifu kamili."

Putin aliyeonekana kuwa na hasira, amewaambia wanasiasa wa Magharibi wakumbuke hatima ya watu kama Adolf Hitler wa Ujerumani ya Kinazi na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa ambao hawakufanikiwa kuivamia Russia katika siku za nyuma.

Tags