Mar 02, 2024 11:50 UTC
  • Wananchi wa Cuba wataka kusimamishwa mauaji ya kimbari Gaza

Wananchi wa Cuba wameungana na mamilioni ya wengine katika maandamano ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, sambamba na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na vita vya mauaji ya kimbari vya utawala dhalimu wa Israel.

Waandamanaji nchini Cuba na katika maeneo mengine ya dunia wamelaani kuendelea uvamizi na mauaji ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza. Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Kuunga Mkono Watu wa Palestina yamefanyika katika miji mbali mbali kote duniani Jumamosi ya leo.

Huko Havana, mji mkuu wa Cuba, waandamanaji walikusanyika katika jengo la José Martí Anti-Imperialist ambalo lipo mkabala na ubalozi wa Marekani katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini kwenye maandamano hayo ya kutetea harakati ya kuikomboa ardhi ya Palestina ambayo inakaliwa kwa mabavu na kukoloniwa na utawala ghasibu wa Israel.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanani hao yalikuwa na jumbe zinazosema: Israel inatekeleza sera ya kuwaangamiza wananchi wa Palestina; ukatili basi, na unyanyasaji basi.

Mmoja wa waandamanaji amenukuliwa na waandishi wa habari akisema: Hakuna kinachoweza kuhalalisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Maandamano ya kulaani jinai za Israel huko Gaza nje ya Ikulu ya White House

Kabla ya hapo, Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba alisema kuwa, mauaji yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza ni Holocaust halisi na ya kweli.

Amesema watu wa Cuba hawatapuuza uhalifu huu na ndiyo maana wameshiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Kuunga Mkono Watu wa Palestina Jumamosi hii.

Tangu kuanza kwa mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023, Wapalestina zaidi ya 30,000, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa shahidi, huku wengine wapatao 70,000 wakijeruhiwa.

Tags