Wairani kufanya maandamano kote nchini kupinga ghasia na fujo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135358-wairani_kufanya_maandamano_kote_nchini_kupinga_ghasia_na_fujo
Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu la Iran limetangaza kuwa, wananchi Waislamu wa Jamhuri ya Kiislamu kesho Jumatatu watafanya maandamano katika pembe zote za nchi kulaani ghasia na fujo zilizochochewa hapa nchini na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-01-11T06:36:11+00:00 )
Jan 11, 2026 06:36 UTC
  • Wairani kufanya maandamano kote nchini kupinga ghasia na fujo

Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu la Iran limetangaza kuwa, wananchi Waislamu wa Jamhuri ya Kiislamu kesho Jumatatu watafanya maandamano katika pembe zote za nchi kulaani ghasia na fujo zilizochochewa hapa nchini na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya baraza hilo imeeleza kuwa, uharibifu wa mali za umma na milki binafsi unaoshuhudiwa hapa nchini unafanyika kwa amri ya Rais Donald Trump wa Marekani akishirikiana na Waziri Mkuu mtenda jinai wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu la Iran limeeleza bayana kuwa, hapa jijini Tehran, wananchi Waislamu wa Iran watakusanyika katika medani mashuhuri ya Enghelab kushiriki maandamano hayo ya amani ya kulaani fujo na ghasia zilizochochewa na Washington na Tel Aviv hapa nchini. 

Taarifa ya baraza hilo imebainisha kuwa, waandamanaji waelewa na wenye ghera ya uhuru na mamlaka imara ya nchi watatenganisha njia yao na ya wachache wanaoitakia mabaya nchi, wafanyao vitendo vya ukatili na kuvuruga nidhamu ya jamii.

Hivi karibuni, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa aliliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akisema Marekani imeyageuza maandamano ya amani ya wananchi wa Iran kuwa ghasia na machafuko.

Iravani amelaani mienendo inayokiuka sheria ya Marekani na ushirikiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuingilia mambo ya ndani ya Iran. Amesema uingiliaji kati huo unafanyika kwa kutumia vitisho, uchochezi wa machafuko na kuvuruga amani na utulivu. Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza akisema: Tunalaani vitendo hivyo vinavyovuruga amani na ambavyo ni kinyume na Hati ya Umoja wa Mataifa.

Kadhalika Baraza la Usalama wa Taifa la Iran mbali na kuashiria kuwa tangu baada ya vita vya siku 12 Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel hazijaacha kufanya chokochoko za vita na uadui dhidi ya taifa la Iran, limesisitiza kwamba: taifa linaloheshimika la Iran litazivunja mbinu za kihujuma na ufanyaji uharibifu wa adui kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.