Mar 06, 2024 03:37 UTC
  • Medvedev: Hakika Ukraine ni sehemu ya Russia, inapasa irudi nyumbani

Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, amesema Ukraine ni sehemu ya nchi hiyo na amefutilia mbali suala la kufanya mazungumzo ya amani na uongozi wa sasa wa Ukraine.

Medvedev ameyasema hayo alipohutubia tamasha la vijana katika mji wa kusini wa Sochi na kusisitiza kuwa Russia itaendeleza kile alichokiita "operesheni maalumu ya kijeshi" hadi upande wa pili utakaposalimu amri.

Rais huyo wa zamani wa Russia aliyewahi vilevile kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo amezungumzia pia kile alichokiita sehemu za kihistoria za Russia ambazo amesema inapasa "zirudi nyumbani".

Medvedev ametoa hotuba hiyo akiwa mbele ya ramani ya Ukraine, ambayo inaonyesha nchi hiyo kama sehemu ndogo sana isiyo na bahari iliyobanwa na Poland huku Russia ikiwa imedhibiti kikamilifu pwani yake ya mashariki, kusini na Bahari Nyeusi.

Huku akishangiliwa na hadhirina, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameendelea kueleza akisema: "mmoja wa viongozi wa zamani wa Ukraine alisema wakati fulani kwamba Ukraine sio Russia. Dhana hiyo inapasa itoweke milele. Hakika Ukraine ni Russia”.

Medvedev ametamka bayana kuwa, haitawezekana kufanya mazungumzo ya amani na uongozi wa sasa wa Ukraine, chini ya Rais Volodymyr Zelenskyy.

Amesema serikali yoyote ya baadaye ya Ukraine ambayo itataka mazungumzo itahitaji kutambua kile alichokiita hali halisi mpya iliyopo.

Akizungumzia uhusiano wa Mashariki na Magharibi, Medvedev amesema uhusiano wa Russia na Marekani umekuwa mbaya zaidi kuliko wakati wa mgogoro wa makombora ya Cuba wa mwaka 1962.../

 

Tags