Rais wa Brazil ataka kuundwa nchi huru ya Palestina
Rais Lula da Silva wa Brazil kwa mara nyingine tena ametangaza himaya na uungaji mkono wake kkwa taifa la Palestina na kusisitiza juu ya kuundwa nchi huru ya Palestina.
Rais wa Brazil akiwa ameshikilia bendera ya Palestina katika hafla ya kitamaduni, alitangaza tena kuwaunga mkono Wapalestina.
Wakati wa sherehe za ufunguzi wa Kongamano la nne la Utamaduni wa Kitaifa huko Brasilia, mji mkuu wa Brazil kwa mara nyingine tena alitoa wito wa kuundwa taifa huru la Palestina na kusisitiza uungaji mkono wake kwa Wapalestina mkabala wa mauaji ya kimbari ya utawala ghasibuu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza zinahesabiwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya karibuni na aghalabu ya jinai hizo zimetajwa kuwa ni maangamizi ya kizazi huku zikilinganishwa na uhalifu ulizofanywa na Adolf Hitler, kiongozi Manazi wa Ujerumani, katika Vita vya Pili vya Dunia.

Hivi karibuni Rais Luis Inacio Lula Da Salva wa Brazil alitahadharisha kuwa kinachojiri katika Ukanda wa Gaza dhidi ya wananchi wa Palestiuna hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi kingine chochote cha historia isipokuwa wakati wa Hitler. Rais wa Brazil alisisitiza kuwa, kile kinachotokea Ukanda wa Gaza si vita bali ni mauaji ya kimbari yanayokumbusha matendo ya Hitler.
Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 30,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 70,000 wamejeruhiwa katika vita vya Israel na Marekani dhidi ya Gaza. Hospitali nyingi na vituo vya matibabu vimelengwa na kuharibiwa kwa mashambulio ya Israel.