Mar 22, 2024 10:57 UTC
  • Viongozi wa EU waionya Israel dhidi ya kuishambulia Rafah

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ufute mpango wake wa kuuvamia na kuushambulia kijeshi kupitia ardhini mji wa Rafah ulioko kusini ya Ukanda wa Gaza.

Viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya wametoa mwito huo baada ya kufanyika mkutano wa Baraza la Mawaziri la EU mjini  Brussels na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kuwepo kwa usitishaji vita kwa misingi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo.

Wamesema kuanzishwa operesheni ya nchi kavu ya Israel dhidi ya Rafah kutalifanya janga la kibinadamu linaloshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza kuwa kubwa na mbaya zaidi.

Aidha viongozi wa EU wamesema uamuzi wa utawala wa Israel kupanua operesheni za kijeshi Gaza hadi mji wa kusini wa Rafah utazuia utoaji wa huduma za msingi na kufikishiwa misaada ya kibinadamu wakazi wa mji huo.

Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitahadharisha Israel kuhusu oparesheni yoyote ya kijeshi katika mji wa Rafah na kusema, misaada ambayo imewasili Ukanda wa Gaza haitoshi kukidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo.

Mgogoro wa kibinadamu Rafah

Kabla ya hapo pia, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema katika Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba, "Aina yoyote ya shambulio dhidi ya Rafah itasababisha maangamiizi ya Wapalestina milioni moja na laki tano walioko katika eneo hilo."

Zaidi ya nusu ya wakazi milioni mbili na laki tatu wa Gaza wamekimbilia Rafah kuepuka hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel katika maeneo mengine, na wamefurika kwenye kambi kubwa za mahema na makazi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa karibu na mpaka.

Tags