Jumatano, tarehe 30 Aprili, 2025
Leo ni Jumatano tarehe Pili Dhulqaada 1446 Hijria sawa na Aprili 30 mwaka 2025.
Tarehe 10 Ordibehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani inafahamika kuwa ni Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi.
Siku hii jina hilo kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuipa majina mengine yasiyo na msingi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson.
Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na ya kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi.

Siku kama ya leo miaka 1135 iliyopita, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokezi wa Hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya 4 Hijria.
Ibn Khuzaima alianza kutafuta elimu katika miji na nchi mbalimbali akiwa bado kijana. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha al Tauhid wa Ithbat Sifatu al-Rab.

Siku kama ya leo miaka 248 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani.
Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mno mwanawe ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo alitabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Tarehe 30 Aprili mwaka 1945 dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, alijiua akiwa mafichoni chini ya ardhi baada na kufeli ndoto yake ya kutawala dunia nzima.
Hitler alizaliwa mwaka 1889 nchini Austria na alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia katika safu za kwanza za askari wa Ujerumani. Adolf Hitler alianzisha chama cha National Socialist German Workers baada ya kuchanganya itikadi za kisoshalisti na mitazamo mikali ya utaifa. Na ulipotimia mwaka 1939 alianzisha Vita vya Pili vya Dunia.
