Kremlin: Umoja wa Ulaya unataka vita, sio mazungumzo
Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin), Dmitry Peskov amesema Umoja wa Ulaya umekuwa ukizuia juhudi za kidiplomasia za Washington na Moscow kwa ajili ya kumaliza mzozo wa Ukraine, na badala yake unafanya jitihada za kurefusha uhasama na mzozo huo.
Peskov asema hayo katika mahojiano na jarida la Ufaransa la Le Point na kuongeza kuwa: EU imeonyesha kuwa haina uhuru, na kwamba "bara zima (la Ulaya)" lilikuwa likimtumia Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden wakati mzozo wa Ukraine uliposhtadi mwaka 2022.
"Mambo yalibadilika baada ya Donald Trump kurejea katika Ikulu ya White House mwezi Januari," Peskov amebainisha, akiongeza kuwa, sasa "Washington inazungumza kuhusu amani" huku "Wazungu wakizungumza tu kuhusu vita."
Moscow na Washington zimefanya duru nyingi za mikutano ya ngazi ya juu mwaka huu iliyolenga kufikia makubaliano ya amani. Wakati huo huo, msimamo wa EU umeonekana kulenga kudhoofisha nafasi yoyote ya mafanikio na amani.
Wakuu wa ulinzi wa Ulaya Magharibi, wakiongozwa na Uingereza na Ufaransa, walikutana mwezi huu kujadili suala la kupeleka kikosi cha "uhakikisho" Ukraine, licha ya onyo kali kutoka Moscow.
Moscow imekuwa ikikosoa mara kwa mara hatua ya EU kuisheheneza Ukraine kwa silaha, na kulaani mipango ya kupeleka wanajeshi nchini huo, ikishutumu umoja huo kwa kujaribu kupanua uwepo wake wa kijeshi na kurefusha mzozo badala ya kutafuta suluhu.
Alipoulizwa iwapo Russia ingelikubali EU kuja katika meza ya mazungumzo, Peskov amejibu, "Hakuna cha kujadili - Ulaya inataka vita, sio mazungumzo. Hatutawalazimisha!"