Kama walivyomfanyia Ozil, mrengo wa siasa kali za kulia Ujerumani watumia kidole cha shahada cha Rudiger kuwashambulia Waislamu
(last modified Sat, 30 Mar 2024 07:38:51 GMT )
Mar 30, 2024 07:38 UTC
  • Kama walivyomfanyia Ozil, mrengo wa siasa kali za kulia Ujerumani watumia kidole cha shahada cha Rudiger kuwashambulia Waislamu

Kundi la siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani limezusha mzozo mkubwa nchini humo baada ya kumhusisha mchezaji wa soka Muislamu wa timu ya taifa ya Ujerumani, Antonio Rudiger, na "makundi ya kigaidi" kwa sababu tu ameonekana kwenye picha ya Instagram akiwa amevaa kanzu nyeupe juu ya mswala, akiinua juu kidole chake cha shahada.

Tuhuma hizo zimetolewa na Julian Reichelt, aliyekuwa mhariri mkuu wa gazeti la Bild, ndipo mchezaji huyo pamoja na Shirikisho la Soka la Ujerumani walipoamua kumfungulia kesi mwandishi huyo wa habari kwa tuhuma zinazomkabili ikiwa ni pamoja na kutoa matamshi ya chuki, kashfa na uchochezi.

Picha hiyo ya Antonio Rudiger iliambatana na maneno: "Ramadan Mubarak kwa Waislamu wote. Mungu atukubalie Saumu na maombi yetu," na ilichapishwa mwanzoni wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hata hivyo, tuhuma za Reichelt hazikutolewa hadi wiki hii, ambapo amehusisha kidole cha shahada cha Rüdiger na kundi la kigaidi la ISIS. 

Mwandishi huyo wa habari amekataa kuomba radhi kwa kumhusisha Rüdiger na ugaidi akisisitiza kwamba, kitendo cha kutoa shahada cha Rüdiger "ni nembo ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na eti wauaji wa Kiislamu duniani kote."

Reichelt anajulikana kwa misimamo yake ya kuiunga mkono Israel anapochapisha jumbe kila siku kwenye mtandao wa X ambazo zinaangazia simulizi rasmi za utawala  huo ghasibu unaoendelea huo kuua watoto wa Palestina.

Julian Reichelt, Mwandishi wa habari Mjerumani mwenye chuki na Uislamu 

Julian Reichelt kwa sasa anafanya kazi katika tovuti ya "News" ya Ujerumani, ambayo ni ya gazeti la mrengo wa kulia, baada ya kufukuzwa katika gazeti la "Bild", kama mhariri wake mkuu kwa sababu zinazohusiana na matumizi mabaya ya mamlaka yake, hasa kuanzisha mahusiano ya kingono na wanawake waliokuwa wakifanya kazi chini ya amri yake.

Abdul Samad Al-Yazidi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani anasema: "Wale walioanzisha kashfa hii wanajua kwa hakika kwamba kuinua kidole cha shahada hakuna uhusiano wowote na kundi la kigaidi la ISIS, bali ni ishara ya imani ya Tauhidi na Mungu Mmoja, lakini wanajaribu kutengeneza migogoro ili kuchochea umma dhidi ya Waislamu."

Rudiger akiinua juu kidole cha shahada

Hii si mara ya kwanza kwa mchezaji Muislamu wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani kushambuliwa kwa sababu ya dini yake. Huko nyuma, viongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany walimshambulia mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo na timu za Arsenal ya Uingereza na Real Madrid ya Uhispania, Mesut Özil, kutokana na picha yake akifanya ibada ya Umrah katika mji mtakatifu wa Makka wakidai kuwa, hayo si maisha yake halisi katika nchi za Magharibi. Baada ya hapo walianzisha propaganda chafu dhidi ya Özil hasa baada ya kukutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, jambo ambalo lilimlazimisha kuchukua uamuzi kustaafu soka ya kimataifa.

Mesut Özil, Masjidul Haram

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani, Al-Yazidi anasema kuwa pande zinavyoshiriki katika kampeni hiyo ya kumchafulia jina mcheza soka Muislamu Antonio Rudiger zina chuki dhidi ya watu wengine na dini nyingine wanazoziona kuwa ni za kigeni, si Waislamu pekee, lakini hazithubutu kuzishambulia dini nyingine kama zinavyofanya dhidi ya Uislamu, kwa sababu hujuma na chuki dhidi ya Uislamu imeruhusiwa sasa hata ndani ya Bunge la Ujerumani.

Abdul Samad Al-Yazidi ameongeza kuwa, mashambulizi dhidi ya Uislamu yanatokea mchana kweupe bila ya kuchukuliwa hatua yoyote dhidi ya vitendo hivyo viovu. Amesema kuendelea kwa jambo hilo kama lilivyo sasa ni hatari kwa jamii inayojumuisha watu wa dini na mbari zote ya Ujerumani.