Azimio la UN lataka Israel iwajibishwe kwa uhalifu wake wa kivita
Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka kusitishwa kwa mauzo yote ya silaha kwa Israel, na utawala huo kuwajibishwa kwa uhalifu wa kivita unaoweza kutokea katika Ukanda wa Gaza.
Azimio hilo lilipitishwa siku ya Ijumaa kwa kura 28 za "ndiyo", sita za "hapana" na nchi 13 hazikupiga kura. Kama ilivyotarajiwa, washirika wakuu wa Israel, Marekani na Ujerumani, walikuwa miongoni mwa waliopinga azimio hilo.
Azimio hilo lenye maneno makali limezitaka nchi "kusitisha uuzaji, uhamishaji na ufikishaji wa silaha, risasi na vifaa vingine vya kijeshi kwa Israel... ili kuzuia ukiukaji zaidi wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukiukwaji wa haki za binadamu."
Pia azimio hilo limesema Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliamua mnamo Januari "kwamba kuna hatari inayowezekana ya mauaji ya kimbari" huko Gaza.
Azimio hilo ambalo liliwasilishwa na Pakistan kwa niaba ya nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) isipokuwa Albania, lilisisitiza "haja ya kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukaji wote wa sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu ili kukomesha hali ya kutokujali. "
Pia azimio hilo limebainisha "wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu."
Azimio hilo pia limetaka "kusitishwa mara moja mapigano" na "kutekelezwa ufikishaji wa dharura wa misaada ya kibinadamu."
Azimio hilo pia limeshutumu "matumizi ya njaa ya raia kama silaha ya vita huko Gaza", ambapo Umoja wa Mataifa umeonya juu ya njaa inayokuja.