Wataalamu waonya: Ongezeko la joto linazidisha hatari za kiafya
Wataalamu wametahadharisha kuwa ongezeko la joto duniani linalohusishwa na mabadiliko ya tabianchi linasababisha kuenea magonjwa zaidi yanayoambukizwa na wanyama, huku maeneo mbalimbali duniani yakiathiriwa na vipindi virefu vya magonjwa ya msimu kama vile mafua.
Dakta Emine Didem Evci Kiraz wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Adnan huko Aydin nchini Uturuki ameeleza kuwa, kuongezeka hali ya joto duniani kunaweza kusababisha ongezeko kubwa la athari za mionzi ya ultraviolet kutoka kwenye jua, kushuhudiwa mabadiliko katika ubora wa vyakula, matatizo ya afya ya akili na kuenea magonjwa yanayosababishwa na wanyama.
Dakta Emine pia amegusia uwezekano wa kutokea magonjwa mapya, akisisitiza kuwa afya ya binadamu ipo hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Amesema, wastani wa joto la mwili kwa binadamu ni kati ya nyuzi joto 36.1 hadi 37.8, na kwamba ongezeko la joto huchagiza utendaji wa moyo na mishipa ya damu, husababisha maji kupungua katika tishu na seli za mwili na huathiri utendaji wa figo.
Wakat huo huo Dakta Emine Didem wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Adnan huko Aydin Uturuki ameeleza kuwa, wanyama wanasambaza magonjwa na maambukizo mapya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Ametaja kushuhudiwa ongezeko la magonjwa mbalimbali kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kama vile maambukizo ya virusi vya Arbo, homa ya dengue, homa ya Chikungunya nk.