Washindi wa Oscar wajiunga na "Cinema for Gaza"
Waigizaji mashuhuri wamejiunga na mnada wa "Cinema for Gaza" ili kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Idadi kadhaa ya wakurugenzi wa filamu na nyota wa tasnia hiyo, wakiwemo waigizaji walioshinda tuzo ya Oscar, Susan Sarandon na Olivia Colman, wamejiunga na mnada wa Cinema kwa Gaza, ambao unachangisha fedha za misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Mnada huo uliozinduliwa mwishoni mwa mwezi uliopita na kundi la watengenezaji filamu na waandishi wa Uingereza, wakiwemo Tilda Swinton, Josh O'Connor na wengineo, na hadi sasa umekusanya zaidi ya pauni 100,000.
Mnada wa "Cinema for Gaza" utaendelea hadi mwisho wa tarehe 12 Aprili.
Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina. Kimya cha jamii ya kimataifa na jumuiya za Kimagharibi za eti kutetea haki za binadamu kimeitia kiburi zaidi Israel kuendeleza mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina.
Zaidi ya Wapalestina elfu 33 wameuawa na wengine zaidi ya elfu 75 kujeruhiwa katika mauaji hayo.