Ireland: Lazima tutatambua uwepo wa nchi huru ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Micheál Martin amesema kuwa haikubaliki hata kidogo kukwamishwa na kucheleweshwa kutambuliwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ireland amegusia pia jinsi nchi yake ilivyowasilisha pendekezo rasmi la kuitambua nchi huru ya Palestina na kusema kuwa, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba hakuna kitu kinachoweza kuizuia nchi yake kutambua uwepo wa nchi huru ya Palestina.
Vile vile amekumbusha kuwa miezi sita nyuma alizungumzia uwepo wa nchi huru ya Palestina na kwamba suala hilo halifai kucheleweshwa hata kidogo.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland yamekuja baada ya serikali ya Uhispania kutangaza kwamba Waziri Mkuu wa nchi hiyo Pedro Sanchez atakutana na baadhi ya viongozi wenzake katika Umoja wa Ulaya wiki ijayo kujaribu kuunga mkono na kulitia kasi na nguvu suala la kutambuliwa rasmi taifa huru la Palestina.
Kabla ya hapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Australia ilikuwa imetangaza kuwa Canberra inalifikiria suala la kutambua uwepo wa taifa huru la Palestina, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanasema ni mabadiliko katika sera za nchi hiyo.
Msemaji wa Serikali ya Uhispania, Pilar Alegria, amewaambia waandishi wa habari kwamba ajenda ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Pedro Sanchez inajumuisha mikutano na mawaziri wakuu wa Norway, Ireland, Ureno, Slovenia na Ubelgiji, na inaangazia msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu vita vya Isarel katika Ukanda wa Ghaza huko Palestina.