Russia yaikosoa vikali Nato kwa kuanzisha mgogoro
Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia jana Jumanne aliwasilisha taarifa na kueleza kuwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) una nafasi kubwa katika kuzua migogoro na kuendeleza hali ya mivutano katika maeneo mbalimbali duniani.
Taarifa ya Zakharova imeeleza kuwa muungano wa Nato hauwajibiki kwa mujibu wa uhalisia wa mambo katika kutathmini vitisho vilivyopo na kwamba unapuuza vitisho vya wazi vilivyopo.
Ukosoaji huo wa Moscow kwa utendaji wa Nato hauhusiani na eneo la Ulaya pekee, bali muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni umechangia pia kushadidisha ukosefu wa amani nje ya eneo lake la kijiografia. Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) si tu kuwa umesababisha hali ya mivutano huko Ulaya Mashariki kwa kushadidisha mikwaruzano baina yake na Russia, bali Nato imekuwa na nafasi hasi pia katika pembe mbalimbali za dunia khususan katika eneo la Mashariki ya Kati kwa hatua yake ya kushirikiana katika mipango na harakati zinazotekelezwa na Muungano wa Kimataifa dhidi ya Daesh huko Syria na Iraq. Lengo la mipango hiyo badala ya kuwa ni kwa ajili ya kulidhoofisha kundi la kigaidi la Daesh, imekuwa ikizidisha uwezo na nguvu ya makundi yanayoipinga serikali ya Syria kwa maslahi ya Marekani. Mfano mwingine wa nafasi hasi ya Nato ni uingiliaji wake kijeshi huko Libya mwaka 2011 uliofanyika kwa kisingizio cha kuanzisha eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege, ambapo Nato ilikuwa na nafasi kuu katika kumpindua Gaddafi dikteta wa zamani wa nchi hiyo na baadaye kusabisha kuongezeka wimbi la ghasia na machafuko nchini humo. Russia inaona kuwa, hatari kuu inayozikabili kwa pamoja nchi wanachama wa Nato na Russia yenyewe ni kuongezeka vitisho vya ugaidi kutoka kundi la Daesh na makundi mengine ya kitakfiri kama harakati ya Jabatul-Nusra. Vitisho hivyo vimezidi kudhihiri hivi sasa kwa kuzingatia kuwepo raia wengi wa nchi za Ulaya na wa Russia pia katika safu ya magaidi na pia kuwepo hofu ya kurejea magaidi hayo katika nchi zao na kutekeleza huko oparesheni za kigaidi.
Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi wa Nato unafanya kila uwezalo ili kuidhihirisha Russia kuwa tishio kuu na hivyo kutuma vikosi vyake mkabala na Russia katika mipaka yake ya magharibi badala ya kushirikiana na Moscow katika vita dhidi ya ugaidi. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameashiria kikao cha wakuu wa nchi 28 wanachama wa Nato huko Warsaw mji mkuu wa Poland na kueleza kuwa Nato ingali iko ndotoni. Nato imeelekeza jitihada zake kwa tishio la kudhaniwa tu yaani Russia, licha ya kutolewa tangazo la kudhamini amani na uthabiti wa Ulaya kwa kushirikiana pande za kimataifa dhidi ya vitisho halisi vilivyopo. Hatua ya Nato ya kutekeleza siasa za kukabiliana na Russia na wakati huo huo kukata ushirikiano na Moscow ni wazi kuwa imedhoofisha jitihada za kimataifa za kuendesha vita dhidi ya ugaidi, mapambano dhidi ya maharamia wa baharini, silaha za maangamizi ya halaiki, biashara ya madawa ya kulevya na ukosefu wa amani katika eneo. Suala jingine lililoshadidisha hisia za Russia ni sisitizo la muungano wa Nato kwa ajili ya kuvuruga mlingano wa nguvu za kijeshi barani Ulaya kupitia utekelezaji wa hatua kama kuwekwa mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora huko Ulaya Mashariki; hatua ambazo zitakuwa na taathira hasi kwa usalama wa eneo. Muungano wa Nato umeonyesha wazi wazi hatua zake dhidi ya Russia kwa kuendelea kutekeleza mipango kama ile ya kutuma batalioni zake nne mpya huko Poland, Lithuania na Estonia.