May 22, 2024 07:06 UTC
  • WHO yatahadharisha kuhusu ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya zinaa

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuhusiana na ongezeko la maambukizi ya maradhi ya zinaa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika hilo ni kwamba, watu zaidi ya milioni 1 huambukizwa magonjwa ya zinaa kila siku ikiwemo kaswende na kisonono.

Ongezeko kubwa zaidi la maambukizi limeshuhudiwa barani Amerika na Afrika.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kuhusu changamoto katika mapambano dhidi ya magonjwa ya zinaa. Kulingana na taarifa ya iliyotolewa na WHO, idadi ya kila mwaka ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa kaswende iliongezeka kutoka karibu milioni 7.1 mwaka 2020 hadi milioni 8 mwaka 2022.

Jumla ya watu 230,000 walikufa kutokana na magonjwa ya bakteria mwaka 2022.

Magonjwa ya zinaa ni miongoni mwa maambukizi yanayofahamika sana na yaliyoleta madhara makubwa hasa katika nchi zinazoendelea ambazo nyingi ziko barani Afrika.

Kulingana na WHO, magonjwa ya zinaa huathiri uwezo wa kujamiiana na uzazi, na huongeza hatari ya ugumba, matatizo ya ujauzito, saratani na VVU/UKIMWI.

Magonjwa ya zinaa hayawezi kuambukizwa kwa kupeana mikono au kugusana, au kugusa nguo au katika viti vya chooni.

Ripoti hiyo pia iligusia kupungua polepole kwa maambukizi mapya ya  Virusi vya Ukimwi (VVU).

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa, nchi nyingi tayari zimeendeleza mikakati ya kiafya ya kuzuia maambukizi ya VVU na kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.