Jun 13, 2024 02:10 UTC
  • Yaliyoifanya Marekani ipendekeze katika Baraza la Usalama la UN azimio la kusitishwa vita Ghaza

Marekani ambayo huko nyuma ilionyesha waziwazi kuwa ndiye muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuyapigia kura ya turufu mara kadhaa maazimio tofauti ya Umoja wa Mataifa ya kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza, hatimaye siku ya Jumatatu Juni 10 iliwasilisha azimio jipya la usitishaji vita ambalo lilipitishwa na Baraza la Usalama kwa kura 14 kati ya 15 zilizounga mkono, ukiondoa Russia tu iliyoamua kutopiga kura.

 
Azimio la usitishaji vita Ghaza lilivyopigiwa kura

Azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusu usitishaji vita katika Ukanda wa Ghaza lilipitishwa bila upinzani wowote wala kupigiwa kura ya turufu katika kikao hicho cha Jumatatu cha Baraza la Usalama. Katika azimio hilo lenye vipengele saba, umetiliwa mkazo umuhimu wa juhudi za kidiplomasia za mtawalia zinazofanywa na Misri, Qatar na Marekani kwa lengo la kuwezesha kufikiwa na kutekelezwa kwa awamu tatu mapatano ya kusitisha vita kikamilifu katika Ukanda wa Ghaza.

 Azimio hilo linasisitiza kuwa iwapo mazungumzo ya awamu ya kwanza yatachukua muda wa zaidi ya wiki sita, usitishaji vita utaendelea maadamu mazungumzo hayo yatakuwa yanaendelea; na linabainisha kuwa Marekani, Misri na Qatar ziko tayari kutoa hakikisho la kuendelezwa mazungumzo hadi makubaliano yatakapoweza kufikiwa juu ya masuala yote na kuanzishwa mchakato wa awamu ya pili. 
Azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama linasisitizia umuhimu wa pande mbili husika kuheshimu masharti ya pendekezo hilo baada ya makubaliano kufikiwa na kuzitaka nchi zote wanachama na Umoja wa Mataifa wenyewe kuunga mkono utekelezaji wake. Azimio hilo linakataa jaribio lolote la kuubadilisha muundo wa idadi ya watu au sehemu yoyote ya eneo Ukanda wa Ghaza. 
Huko nyuma Marekani ilipigia kura ya veto maazimio kadhaa ya kusitisha vita Ghaza

Marekani ambayo huko nyuma ilionyesha waziwazi kuwa ndiye muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuyapigia kura ya veto mara kadhaa maazimio ya Umoja wa Mataifa, imelazimika kuchukua hatua hiyo sasa hivi na katika kipindi hiki nyeti na hasasi kwa sababu kadhaa.

 
Sababu ya kwanza ni kuwepo hali tete ndani ya utawala wa Kizayuni na kuibuka migogoro kadhaa katika utawala huo; na kwa hiyo lengo mojawapo la kupendekezwa usitishaji vita ni kuutoa utawala huo kwenye lindi la hali hiyo ya sasa. Ukweli ni kuwa utawala wa Kizayuni sasa hivi unakabiliwa na hali tete zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Benny Gantz na Gadi Eisenkot wamejiuzulu kwenye baraza la mawaziri la vita. Haley Trooper, ambaye ni mmoja wa watu walio karibu na Gantz, ametangaza rasmi kujiondoa kwenye baraza la mawaziri la mseto linaloongozwa na Netanyahu. Kwa hiyo, hali tete ya kisiasa na kijeshi ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu imefikia kiwango cha juu kabisa; na kwa hiyo kupitishwa azimio la kusitisha mapigano Ghaza kunaweza kuwa fursa ya kufifisha na kuficha hali hiyo tete ndani ya utawala wa Kizayuni.
Biden na serikali yake wamehusika moja kwa moja katika mauaji ya maelfu ya Wapalestina wasio na hatia Ghaza

Sababu ya pili ni hitajio kubwa alilonalo Joe Biden na serikali yake la kushawishi na kuvutia maoni ya umma ndani ya Marekani wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ili kuziteka fikra za Wamarekani kwa kujionyesha kuwa na sura ya ubinadamu. Katika miezi ya hivi karibuni yamefanyika maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na kulaani sera za Marekani kuhusiana na utawala wa Kizayuni, ambapo maandamano ya wanafunzi yaliyoungwa mkono hata na wahadhiri wa vyuo vikuu vya Marekani ni miongoni mwa maandamano muhimu zaidi. Serikali ya Biden imeandamwa na mbinyo na mashinikizo makubwa ya waandamanaji wakati muda uliosalia si mwingi hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo. Nia ya Biden na timu yake ni kujaribu kulitumia azimio la kusitisha mapigano huko Ghaza kwa maslahi na malengo yao ya kisiasa.

 
Sababu nyingine muhimu ni kwamba hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliliweka jina la utawala wa Kizayuni kwenye orodha nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto. Utawala wa Kizayuni umefanya jinai za kutisha dhidi ya watoto wa Ghaza kwa uungaji mkono wa Marekani. Kwa kufanikisha kupitishwa azimio la kusitisha vita huko Ghaza, Marekani inajaribu kupunguza mashinikizo yanayoiandama kimataifa na ukosoaji mkali unaofanywa dhidi yake.
Muqawama unaendelea kuwachachafya Wazayuni Ghaza na kwengineko

Sababu nyingine ya Marekani kuchukua uamuzi wa kupendekeza azimio la kusitisha vita huko Ghaza ni operesheni za mafanikio na zenye taathira kubwa za Muqawama na kusimama kwake kidete kusimamia masharti yake, jambo ambalo limeuweka kwenye hali ngumu utawala wa Kizayuni na kuifanya Washington ilazimike kukubali usitishaji vita ili kunusuru uhai wa utawala huo bandia. Hata hivyo kwa kuzingatia rekodi yake ya huko nyuma na ya hivi sasa utawala huo ghasibu hautegemewi hata kidogo kuwa utaheshimu kanuni na sheria za kimataifa.

 
Nukta muhimu ni kwamba mwenendo ulioonyesha utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi cha miezi minane iliyopita umethibitisha kuwa utawala huo hautilii maanani wala hauujali hata chembe Umoja wa Mataifa na maazimio ya Baraza lake la Usalama. Maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayouhusu utawala wa Kizayuni hayana hakikisho la utekelezaji, kwa sababu hadi sasa Israel haijawahi kutekeleza azimio lolote lile, zaidi ya kuyafanya maazimio hayo yaonekane kuwa kitu cha maonyesho na propaganda tu.../

 

Tags