Jun 18, 2024 10:32 UTC
  • Putin: Njama za Magharibi za kujaribu kuidhibiti Russia zimefeli

Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa, njama zote za madola ya Magharibi za kutaka kuifanya Moscow itengwe kimataifa zimefeli.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la FARS ambalo limemnukuu Putin akisema: "Si muhimu kwetu wamefanya njama kubwa kiasi gani, lililo muhimu kwetu ni kwamba njama zao zote za kutaka kuifanya Russia itengwe, zimefeli." 

Rais wa Russia ametoa matamshi hayo leo Jumanne kujibu njama za Magharibi dhidi ya Russia.

Matamshi hayo yamenukuliwa pia na gazeti la Rodong Sinmun la Korea Kaskazini wakati huu wa kukaribia zaira ya Putin nchini humo.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais wa Russia amesema: Tunaendelea bila ya kusita na juhudi zetu za kukuza nguvu zetu za kiuchumi, kustawisha sekta za viwanda na teknolojia pamoja na kutia nguvu miundombinu, elimu na utamaduni wetu. 

Safari ya siku mbili ya Rais wa Russia huko Korea Kaskazini imeanza leo Jumanne kwa shabaha ya kuimarisha udugu na urafiki baina ya Moscow na Pyongyang. 

Mwezi Septemba mwaka jana, Kiongozi wa Korea Kaskazinim Kim Jong Un, alifanya ziara nchini Russia na kumwalika Vladmir Putin kuitembelea nchi yake wakati wowote atakapopata nafasi.