Colombia yawataka wakaazi wa utawala wa Kizayuni wapinge jinai za Netanyahu
Rais wa Colombia amewataka walowezi wa Kizayuni kusimama dhidi ya jinai na mashambulizi ya jeshi la utawala katili wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanachuo wa Iran (ISNA), Rais wa Colombia, Gustavo Petro ametoa mwito huo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X sambamba na kusambaza picha za shambulio la Wazayuni kwenye jengo walilokuwa wakiishi raia wa Palestina huko Ghaza na kuwaambia Waisraeli waendeshe harakati za kupinga jinai hizo za Benjamin Netanyahu na jeshi lake.
Katika ujumbe wake huo, rais wa Colombia amewaambia wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel kwamba, fanyeni chochote kinachohitajika ili kuzuia mauaji ya halaiki ya watoto huko Ghaza.
Mwezi uliopita wa Mei pia, Rais Petro alitangaza kuwa nchi yake ya Colombia itavunja uhusiano na utawala wa Kizayuni kutokana na jinai zake huko Ghaza.
Rais wa Colombia alimkosoa vikali waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na kusema kuwa, Colombia inaungana kesi ilivyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICJ.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ghaza, idadi ya raia wa Palestina waliouawa shahidi hadi hivi sasa kutokana na mauaji ya kikatili yanayoendelea kufanywa na Israel huko Ghaza, Palestina imepindukia 37,000 huku idadi ya waliojeruhiwa ikiwa ni zaidi ya 85,000.