Trump ajeruhiwa kwa risasi mkutanoni Pennsylvania; asema yupo salama
Raisi wa zamani wa Markani, Donald Trump, na mgombea wa sasa wa kiti cha rais nchini humo jana alijeruhiwa kwa rsasi akiwa katika mkutano wa hadhara huko Butler, katika jimbo la Pennsylvania akihutubia wafuasi wake; hatua iliyoipelekea timu yake ya ulinzi kumtoa katika sehemu ya tukio.
Ripoti zinasema kuwa milio kadhaa ya risasi ilisikika katika mkutano huo wa Trump jana huko Pennsylvania.
Video ya moja kwa moja kutoka eneo la tukio ilimuonyesha Trump akivuja damu upande wa kulia wa uso na sikio lake. Trump Alionekana akishikilia mkono wake sikioni kabla ya kuanguka chini nyuma ya jukwaa.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa kampeni yake ilieleza kuwa Donald Trump anaendelea vizuri na anapatiwa huduma za matibabu katika kituo cha afya.
Kwa upande wake Donald Trump baadaye alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii akisema kuwa: "Nilipigwa risasi iliyopenyeza sehemu ya juu ya sikio langu."
Wakili wa Wilaya ya Butler, Richard Goldinger, amesema kuwa watu wawili wamepoteza maisha katika tukio hilo la ufyatuaji risasi, akiwemo mtu aliyefyatua risasi. Wakati huo huo duru moja imeliambia shirika la habari la Reuters kuwa aliyefyatua risasi ameuawa na kwamba idara husika ya usalama ya Marekani inachunguza kama ufyatuaji risasi huo ulikuwa jaribio la mauaji au la.
Wafuasi wa Trump na baadhi ya watu wamelitaja tukio hilo kuwa ni jaribio la kutaka kumuuwa mgombea wao.
Uchaguzi wa Rais nchini Marekani umepangwa kufanyika mnamo Novemba 5, mwaka huu 2024. Trump tayari amepata idadi muhimu ya kura za awali ili kuwania uteuzi wa chama cha Republican.
Rais Joe Biden, anayewania kuchaguliwa tena, alishinda mchujo katika chama chake cha Democrats huko New Jersey na Washington, DC, katika baadhi ya mashindano ya mwisho mwezi Juni uliopita mwaka huu.