Amnesty International: Waislamu wa Ufaransa wananyimwa nafasi ya kupumua na wanabaguliwa
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa kuwazuia wanariadha wa Ufaransa wanaovaa vazi la Hijabu kushiriki katika Michezo ya Olimpiki kunakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu, na kunafichua unafiki na baguzi wa serikali ya Ufaransa, na udhaifu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki.
Haya yamesemwa katika ripoti mpya yenye kichwa cha maneno: "Hatuwezi Kupumua Tena, Hata Michezo Hatuwezi Tena", inayokosoa ukiukaji wa haki za binadamu za wanawake na wasichana wa Kiislamu na marufuku ya Hijabu katika michezo nchini Ufaransa.
Ripoti hiyo - iliyochapishwa kabla ya kuanza michezo ya Olimpiki ya Paris - inaelezea athari mbaya zinazosababishwa na marufuku ya vazi la Hijabu kwa wanawake na wasichana wa Kiislamu katika viwango vyote vya michezo nchini Ufaransa.
Anna Bloss, mtafiti wa kimataifa wa haki za wanawake katika Amnesty International amesema: "Kuwazuia wanariadha wa kike wa Ufaransa kushiriki katika mashindano ya Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki wakiwa na vazi la Hijabu kunakadhibisha madai kwamba Paris 2024 ni michezo ya kwanza ya Olimpiki yenye usawa wa kijinsia, na kunaanika wazi ubaguzi wa kijinsia uliopo."
Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema kuwa sheria za kibaguzi zinazoainisha mavazi ya wanawake ni ukiukaji wa haki za binadamu za wanawake na wasichana wa Kiislamu, na zina athari haribifu katika ushiriki wao kwenye michezo, na hivyo kukwamisha juhudi za kuifanya michezo kuwa jumuishi zaidi na kwa ajili ya wote.
Amnesty International imethibitisha kwamba kupigwa marufuku vazi la Hijabu katika michezo mingi nchini Ufaransa "kumesababisha hali isiyoweza kutetewa ambapo nchi mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki inakiuka majukumu yake mengi kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, pamoja na majukumu na maadili yaliyoainishwa katika haki za binadamu za Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki.