Joe Biden ajitoa kwenye kinyang'anyiro cha Urais
Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kujitoa katika mbio za kutetea kiti chake cha urais baada ya kuongezeka mashinikizo ya kumtaka ajiondoe kutokana na sababu mbalimbali likiwemo suala la afya na uwezo wake wa kukumbuka mambo.
Biden jana alithibitisha kuwa hatogombea tena katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba dhidi ya Donald Trump, baada ya mashinikizo kuzidi ndani ya chama chake cha Democratic.
Rais Biden ametangaza kuwa, anakaa kando kutoka kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Marekani 2024. "Imekuwa heshima kubwa maishani mwangu kuhudumu kama rais wenu," alisema kwenye chapisho la mtandaoni.
"Na ingawa imekuwa nia yangu ya kutaka kuchaguliwa tena, naamini ni kwa manufaa ya chama changu na nchi yangu mimi kukaa pembeni."
Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 amekuwa akikabiliwa na mwito wa kusitisha kampeni tangu mdahalo dhidi ya Donald Trump wiki tatu zilizopita, ambapo alionekana kuwa dhaifu, akipambana kueleweka.
Kabla ya taarifa ya Jumapili, Biden alijaribu kuonyesha kupinga na kutupilia mbali miito hiyo na kusisitiza kugombea tena nafasi hiyo kwa ajili ya kutetea muhula wake wa pili.
Baada ya kuthibitisha kuwa anajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, Biden alimuidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi yake. Alisema kumchagua Harris kama makamu wa rais ulikuwa "uamuzi bora zaidi ambao nimefanya".
"Leo nataka kumuunga mkono kikamilifu na kumuidhinisha Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu. Wanademokrati - ni wakati wa kuja pamoja na kumshinda Trump," aliandika Biden. "Hebu tufanye hivi."