Waandaaji: Maandalizi ya michezo ya Olimpiki Paris yamekamilika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i114340-waandaaji_maandalizi_ya_michezo_ya_olimpiki_paris_yamekamilika
Rais wa kamati ya maandalizi ya Olimpiki ya Paris Tony Estanguet amesema kuwa, mji huo uko tayari kwa Michezo hiyo huku akipuuza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakaazi na wafanyabiashara kuhusu athari za tamasha hilo la kimataifa.
(last modified 2024-07-22T03:44:46+00:00 )
Jul 22, 2024 03:44 UTC
  • Waandaaji: Maandalizi ya michezo ya Olimpiki Paris yamekamilika

Rais wa kamati ya maandalizi ya Olimpiki ya Paris Tony Estanguet amesema kuwa, mji huo uko tayari kwa Michezo hiyo huku akipuuza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakaazi na wafanyabiashara kuhusu athari za tamasha hilo la kimataifa.

Sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki itafanyika Ijumaa ijayo. Matayarisho ya mwisho mwisho yanafanywa katika maeneo yote yatakayotumika kwa michezo hiyo na maelfu ya wanamichezo na maafisa wanaendelea kumiminika mjini humo. Operesheni kubwa ya usalama kwa ajili ya hafla ya ufunguzi wa Michezo hiyo inasababisha msuguano, huku sehemu kubwa za katikati ya mji mkuu Paris kwenye kingo za mto huo na karibu na viwanja vya Olimpiki zikifungwa kwa umma.

Vyama vya wafanyabiashara vinavyowakilisha maduka ya Paris, migahawa, na vilabu vimelalamika kuwa vinakabiliwa kudodora kwa biashara, vikilaumu kwa sehemu hatua kali za usalama zilizowekwa.

Hijabu michezoni

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, vyama vya michezo na makundi ya haki za binadamu hivi karibuni yalitoa wito kwa rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach kusaidia kubatilisha marufuku ya wanamichezo wa Ufaransa kuvaa hijabu.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa, marufuku ya hijabu kwa wanamichezo wa Ufaransa inadhoofisha maadhimisho ya mwanzo ya Olimpiki ya usawa wa kijinsia.

Shirika la Amnesty International na makundi mengine 10 yaliotia saini barua ya Mei 24 kwa Bach, yanasema marufuku hiyo ni kinyume na Mkataba wa Olimpiki  na ni sehemu ya suala kubwa kuhusu ubaguzi dhidi ya wanamichezo wa wa kike wa Kiislamu katika ngazi zote za nchini Ufaransa.