Mahakama ya Bangladesh yaondoa sheria ilioibua maandamano ya nchi nzima
Hatimaye Mahakama ya Bangladesh imeondoa sheria yenye utata ya ajira ambayo iliibua maandamando ya nchi nzima na kusababisha makumi ya watu kuuawa katika makabiliano yao na polisi.
Mahakama ya Bangladesh jana Jumapili iliondoa sheria yenye utata kwenye mfumo wa utaoji ajira za serikali, hatua ambayo ni ushindi kwa wanafunzi baada ya siku kadhaa za maandamano ya kitaifa. Wanafunzi wanaolalamikia ukosefu wa ajira wamekuwa wakilalamikia sheria inayohifadhi asilimia 30 ya ajira za serikali kwa ndugu na familia za wanajeshi waliopigana vita vya uhuru wa Bangladesh vya 1971.
Sheria hiyo ilisimamishwa kwa muda mwaka 2018, baada ya maandamano ya wanafunzi, lakini Juni mwaka huu mahakama iliirejesha, na kupelekea maandamano ya kitaifa. Maandamano hayo yamekuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Bangladesh tangu waziri mkuu Sheikh Hasina, kushinda muhula wa nne mfululizo Januari mwaka huu, zoezi ambalo lilisusiwa na vyama vikuu vya upinzani.
Vyuo vikuu vimefungwa kote nchini Bangladesh kufuatia maandamano hayo, huku huduma za intaneti zikikatwa, pamoja na watu kutakiwa kubaki nyumbani.
Kutokana na kutokuweko na mawasiliano, haijabainika iwapo wanafunzi waliokuwa wakigoma wameridhishwa na uamuzi huo wa mahakama au la. Hadi sasa serikali haijatoa idadi ya watu waliokufa kutokana na maandamano hayo yalioanza mwanazoni mwa wiki, lakini magazeti manne nchini yameripoti idadi ya zaidi ya watu 100.