Japan yawawekea vikwazo walowezi Waisraeli kutokana na jinai dhidi ya Wapalestina
Japan kwa mara ya kwanza imewawekea vikwazo walowezi wanne Wazayuni Waisraeli kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Akibainisha kuwa vitendo vya ukatili vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi vimeongezeka kwa kasi tangu Oktoba 2023, Katibu Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Japan Yoshimasa Hayashi amesema leo Jumanne nchi yake imeamua kuwekea vikwazo vya kufungia mali za walowezi wanne wa Kizayuni wanaohusika na vitendo vya ukatili.
Hayashi amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba vitendo kama vile vurugu, vitisho na uharibifu wa mali vinavyofanywa na walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali dhidi ya jamii za Wapalestina na wengine vimekuwa tatizo kubwa, kwani mara kwa mara huua na kuwajeruhi wakazi wa Palestina au kuwalazimisha kuondoka makwao.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inakuja kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi za G7 na nyinginezo. Amesema Japan itatekeleza kwa kasi hatua za kufungia mali na kuendelea kuitaka Israel "kusimamisha kabisa shughuli za makazi kwa ushirikiano na jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na G7."
Hii ni mara ya kwanza kwa Japan kuweka vikwazo dhidi ya walowezi wa Israel. Zaidi ya Waisraeli 700,000 wanaishi kama walowezi katika zaidi ya vitongoji 270 vilivyojengwa tangu mwaka 1967 na utawala wa haramu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki.
Wakati makaazi yote ya walowezi wa Israel ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa, utawala ghasibu wa Israel umeongeza upanuzi wa makazi hayo katika ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hatua hiyo ya Japan imekuja kufuatia uamuzi wa mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa, ICJ, wa kupinga uwepo wa Israel katika ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967.
Siku ya Ijumaa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilisema "kuendelea kuwepo Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria," na kuongeza kuwa utawala huo "unawajibika" kukomesha dhulma hiyo "haraka iwezekanavyo."
ICJ pia imeyataka mataifa yote na mashirika ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, "kutotambua kuwa ni halali" hali inayotokana na kuwepo kinyume cha sheria kwa Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.