Watu 350 waaga dunia katika maporomoko ya ardhi nchini India
Idadi ya watu walioaga dunia nchini India baada ya jimbo la Kerala kukumbwa na janga la kimaumbile na maporomoko ya ardhi imeongezeka na kkufikia 350.
Ripoti zinasema kuwa, takriban watu 350 wamefariki na wengine 100 hawajulikani waliko huko Wayanad, nchini India. Eneo hilo la milima lilikumbwa na maporomoko ya ardhi na mafuriko wiki hii kutokana na mvua za masika.
Lakini idadi hiyo inaweza kubadilika haraka, kwani "mamia ya watu wamenaswa," jeshi limesema, na kuongeza kuwa wengine 250 waliokolewa kati ya matope na uchafu.
Watu wa Kerala wanafuatilia kwa karibu juhudi za uokoaji ambazo zimewezesha kupata zaidi ya watu 1,000 na wanaandaa michango kwa mshikamano na wakaazi wa Wayanad. Wataalamu wanatafuta kuelewa tukio hili baya, kama vile Gireesh Gopinath, mtaalamu wa hali ya hewa katika Chuo Kikuu cha Kerala.
Shughuli za uokoaji zinaendelea, lakini zinatatizwa na mvua kubwa na kuporomoka kwa daraja muhimu. Timu za serikali na za kitaifa zinaendesha shughuli za uokoaji. Wenyeji kadhaa pia wamekuwa wakisaidia.
Waziri wa Haki wa Jimbo la Kerala M.B Rajesh amesema kuwa, jumla ya watu zaidi ya 250 wameokolewa hadi sasa, Gazeti la The Hindu limeripoti.
Miili bado inapatikana kwenye njia za maji, huku video zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha barabara nzima zikisombwa na maporomoko ya matope yaliyobeba uchafu na vigogo vya miti. "Hali ni ngumu sana, kila mtu anazungumza kuhusu miili inayopatikana hapa na pale," Yousuf, ambaye anaishi katika kijiji cha Chooralmala, ameziambia duru za habari.