Independent: Nini kinatokea Uingereza? Waislamu wanadungwa visu, misikiti imezingirwa
Gazeti la The Independent linalochalishwa nchini Uingereza limeripoti kuwa ghasia katika miji kama vile Liverpool, Leeds na Belfast ziligeuka kuwa machafuko makubwa mwishoni mwa juma, wakati watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia walipopigana na polisi wa kutuliza ghasia, huku kukiripotiwa matukio mengi ya mashambulizi dhidi ya kaumu za waliowachache hususan Waislamu katika mitaa ya miji kadhaa ya nchi hiyo.
Katika ripoti mbili tofauti, gazeti hilo limeeleza mlolongo wa ghasia zilizoikumba Uingereza kuwa ni hujuma za kibaguzi. Limeongeza kuwa, madai ya uongo yaliyoenezwa kwenye mtandao yamechochea hisia za chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi, kwa kudai kuwa mshukiwa wa mauaji ya wasichana watatu katika jiji la Southport (kaskazini-magharibi mwa Uingereza) alikuwa Mwislamu anayetafuta hifadhi na kwamba aliwasili nchini humo kwa boti.
Mji wa Southport, karibu na jiji la Liverpool, ulishuhudia makabiliano makali siku chache zilizopita kati ya kundi la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na polisi wa Uingereza nje ya Msikiti wa Southport Islamic Society. Msikiti huo ulizingirwa wakati ghasia zilipozuka Jumanne jioni, na zaidi ya maafisa 50 wa polisi walijeruhiwa huku washambuliaji wenye siasa kali za mrengo wa kulia wakitoa nara za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Gazeti hilo limeripoti kuwa, picha za kushtua zimeonyesha mtu mwenye asili ya Afrika akishambuliwa na kundi kubwa la wazungu wenye msimamo mkali katika Bustani ya Manchester ambako alibagwa chini na kupigwa mateke kabla ya kuokolewa na polisi.
Katika tukio tofauti katika mji huo, wasichana 3 wa Kiislamu wametemewa mate na wazungu waliowashambulia wakitaka kuwavuliwa vazi lao la hijabu.
Katika kituo cha treni cha Liverpool, mwanamume Mwislamu alidungwa kisu, na dereva wa teksi alishambuliwa katika eneo la Hull na watu ambao walikuwa akitoa nara za ubaguzi wa rangi.
Awali, televisheni ya BBC News wa Uingereza umeripoti kuwa mshukiwa wa mauaji ya wasichana watatu katika mji wa Southport ni mzaliwa wa Cardiff na kwamba alihamia eneo la Southport mwaka 2013 na wala si mhajiri Muislamu muomba hifadhi kama ilivyodaiwa.