Aug 06, 2024 02:57 UTC
  • Erdogan: Mauaji ya Haniyeh ni kitendo kiovu, mfumo wa dunia umefilisika

Rais wa Uturuki, Recep Erdogan, alisema jana Jumatatu kwamba mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Israel dhidi ya Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), ni kitendo kiovu ambacho kimetikisa dhamiri za walimwengu, akisisitiza kwamba mfumo wa kimataifa umefilisika mbele ya kile kinachotokea katika Ukanda wa Gaza.

Erdogan alisema - katika hotuba yake kwenye kongamano la haki za binadamu lililoandaliwa na Chama cha Haki na Maendeleo katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara - kwamba mauaji ya kimbari yanayofanywa dhidi ya watu wa Gaza hayawezi kuelezeka kwa maneno na kwamba Israel sio tu inaua watu wa Gaza kwa risasi na mabomu, lakini pia kwa njaa na kiu.

Gaza

Erdogan ameongeza kuwa "mfumo wa dunia unakabiliwa na ombwe hatari la madaraka na tunakabiliwa na kuzorota kwa maadili na dhamiri duniani kote." Amesema kwamba mfumo huu wa dunia "imeinua juu bendera ya kujisalimisha mbele ya kinachotokea Gaza, ambacho kingepaswa kuamsha dhamiri za ubinadamu,” lakini kinyume chake “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijachukua hatua yoyote.”

Kuhusu hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Bunge la Congress huko Marekani, Rais wa Uturuki amesema kwamba "mahali pa asili pa wahalifu wa mauaji ya kimbari sio majukwaa ya bunge bali vyumba vya mahakama."

Erdogan ameongeza kuwa wale waliopigia makofi uongo wa Netanyahu, ambaye kwa mara nyingine tena amemtaja kuwa Hitler wa zama hizi, hawataweza kufuta doa jeusi mikononi mwao.

Erdogan hapo awali alishutumu jinsi Congress ya Marekani ilivyomkaribisha "bila aibu" Benjamin Netanyahu, ambaye alisema "mikono yake imejaa damu ya Wapalestina."