Aug 09, 2024 07:43 UTC
  • Sanders: Wamarekani hawaungi mkono vita vya kikatili vya Netanyahu

Seneta moja mashuhuri nchini Marekani kwa mara nyingine ametoa mwito wa kusitishwa vita mara moja katika Ukanda wa Gaza akisisitiza kuwa, wananchi wa Marekani hawaungi mkono jinai na vita vya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel dhidi ya wakazi wa eneo hilo la Palestina lililozingirwa na linalokaliwa kwa mabavu.

Bernie Sanders, Seneta wa jimbo la Vermont amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: "Watu wa Marekani hawaungi mkono vita vya kutisha vya Netanyahu. Lazima tukikumbushe chama cha Democratic kwamba, iwapo wanataka vijana kujihusisha na mchakato wa kisiasa, lazima wabadili mtazamo wao kwa Gaza.”

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akitoa wito wa kusitishwa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni kwa muda mrefu sasa, amesisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza, ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, karibu raia 40,000 wa Palestina wameuawa shahidi kwa mabomu na makombora ya Wazayuni katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

Netanyahu, nduli wa vita mfyonza damu

Sanders, ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto wa Marekani amebainisha kuwa, Washington inabeba dhima ya mauaji ya kutisha yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo lililozingirwa la Ukanda wa Gaza.

Seneta huyo wa kujitegemea wa Marekani amekuwa akisisitiza kuwa, serikali ya Washington ni mshirika katika jinai za kutisha za Israel huko Ukanda wa Gaza kutokana na uungaji mkono wake kwa utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

 

Tags