Rais Pezeshkian: Iran haitaingia katika mazungumzo chini ya mashinikizo, vitisho na mzingiro
-
Rais Pezeshkian na Shehbaz Sharif
Rais Masoud Pezeshkian amekosoa utata na mgongano unaoshuhudiwa kati ya mbinu za mashinikizo zinazotumiwa na Marekani dhidi ya Iran na kile kinachotajwa kuwa ni nia yake ya kushiriki katika mchakato wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu.
Rais Pezeshkian ametoa matamshi hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistani, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa ikishiriki katika upatanishi kati ya pande hizo mbili.
"Mkanganyiko huu umeongeza kiwango cha kutoaminika [Washington] miongoni mwa watu wa Iran na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu," amesema Rais Pezeshkian.
Ameongeza kuwa: "Kuendelea hatua za uadui za Marekani, ikiwa ni pamoja na mzingiro wa baharini, hakuendani na madai yake ya kutaka kutatua mzozo uliopo kwa njia za kisiasa, na mgongano huu unaidisha hali ya kutoaminiwa Washington baina ya wananchi na viongozi wa Iran.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba njia ya mazungumzo inaweza kuwa na matokeo yanayoonekana wakati upande wa pili utakapotumia mbinu ya kujenga uaminifu na kuheshimiana, badala ya sera ya vitisho, mashinikizo na kutwisha matakwa yake; kwa sababu Iran, ndani ya mfumo wa kanuni zinazotambulika za sheria za kimataifa, inasisitiza umuhimu wa kupata haki halali za watu wake.
Rais ameishauri Washington kwamba, ili kuunda mazingira ya kutatua masuala ya kudumu, kwanza inapaswa kuondoa vikwazo vya kiutendaji kama mzingiro huo.
"Jamhuri ya Kiislamu haitaingia katika mazungumzo chini ya mashinikizo, vitisho au mzingiro," amesisitiza Rais Masoud Pezeshkian.