Russia yatungua makumi ya droni za Ukraine katika anga yake
Russia imetungua makumi ya droni za Ukraine zilizokuwa zikiruka katika anga yake usiku wa kuamkia leo.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga imetungua droni 35 za Ukraine zilizokuwa zikiruka katika majimbo ya Kursk, Voronezh, Belgorod, Bryansk na Oryol huko Russia.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi wa Russia imesema imesambaratisha hatua za serikali ya Kiev za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya Tochka- U dhidi ya maeneo mbalimbali katika ardhi ya Shirikisho la Russia.
Jumanne iliyopita vikosi vya ulinzi vya Ukraine vilitekeleza shambulio la kushtukiza katika ardhi ya Russia. Serikali ya Kiev iliitaja hujuma hiyo kuwa shambulio kubwa zaidi kuwahi kufanyika katika ardhi ya Russia tangu kuanza vita vya Ukraine mwezi Februari mwaka juzi.
Katika hujuma hiyo, vikosi vya ulinzi vya Ukraine vilivuka mpaka na kuingia Russia na kufanya shambulio katika mkoa wa Kursk na kuteka vijiji kadhaa. Rais Vladimir Putin wa Russia amelitaja shambulio hilo la Ukraine lililofanyika kwa msaada wa Marekani kuwa ni "uchochezi mkubwa."
Tangu Februari 2022, nchi za Magharibi zimeipatia Ukraine silaha na zana mbalimbali za kijeshi ili kusaidia vikosi vya Kiev dhidi ya Russia.