Uhaba wa dawa unavyotishia maisha ya wagonjwa nchini Sudan
-
Wagonjwa Sudan
Utafutaji wa dawa za binadamu nchini Sudan umegeuka kuwa maumivu ya kila siku yanayotishia maisha ya maelfu ya watu, huku kukiwa na uhaba mkubwa wa dawa muhimu na kuzagaa ovyo dawa zisizojulikana asili na ubora wake.
Ripoti zinasema kwamba mgogoro huo sasa hauhusu upatikanaji wa dawa tu, bali pia kuhusu usalama wake, na kwamba baadhi ya dawa zinaweza kuwa zimeisha muda wake au kuharibika kutokana na kuhifadhiwa mahali pasipofaa; wakati wagonjwa wakilazimika kutumia dawa yoyote inayopatikana kwa kuhofia afya zao.
Vita vya ndani nchini Sudan vimeathiri vibaya sekta ya dawa, na kampuni nyingi za dawa zimeacha uzalishaji huku minyororo ya usambazaji ikiharibiwa, na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa aina nyingi za dawa, hasa dawa za kuokoa maisha.
Mtaalamu wa sekta ya dawa, Yasser Ahmed Youssef, anasema kwamba Sudan imepoteza kiasi kikubwa cha dawa za magonjwa sugu na hali mbaya, ikiwa ni pamoja na dawa za kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya damu, pamoja na dawa za watoto, akieleza kuwa mgogoro huo unazidi kuwa mgumu kutokana na kuendelea vita na kuvurugika shughuli za uagizaji na usambazaji wa dawa.
Maduka ya dawa nchini Sudan bado yanaonyesha ukubwa wa mgogoro unaoongezeka, huku wagonjwa wakisimama kila siku mbele ya rafu zilizo karibu tupu.
Kwa sasa kuna hofu kwamba kuongezeka uhaba wa dawa na ukosefu wa usimamizi utakuwa tishio la ziada kwa maisha ya raia katika nchi hiyo iliyochoshwa na vita ambapo migogoro ya kibinadamu inaongezeka siku hadi siku.