Wacyprus Kusini waandamana kupinga kushamiri kuwepo kijeshi Marekani katika nchi yao
Aug 11, 2024 23:37 UTC
Vyama vya upinzani katika eneo linaloendeshwa na Ugiriki la Cyprus Kusini (GCASC) vimeelezea kutoridhishwa na ongezeko la uwepo wa jeshi la Marekani, vikiashiria safari za kutembelea bandari za nchi hiyo zinazofanywa na manowari za Washington kwa kuzingatia hali inayoaendelea katika Ukanda wa Ghaza.
Manowari ya Marekani iliyowasili kisiwani humo siku ya Ijumaa ilikabiliwa na maandamano ya upinzani.
Taarifa ya chama kikuu cha upinzani cha mrengo mkali wa kushoto cha Progressive Party of Working People (AKEL), imeashiria kuongezeka misururu ya manowari za Marekani zinazoelekea Kusini mwa Cyprus na kuishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kukiingiza kisiwa hicho kwenye mivutano mikubwa ya kiusalama kwa kuruhusu vikosi vya kijeshi vya kigeni kukusanyika kisiwani humo.
Sehemu moja ya taarifa ya AKEL imesema: "mazingira magumu na ya kutia wasiwasi, ya vita katika eneo hili yanachochea hatari kubwa sana kwa usalama wa mataifa na watu wote wa Mashariki ya Mediterania na Mashariki ya Kati. Kanda yetu nzima inakabiliwa na hatari ya moto wa vita unaosambaa na wenye matokeo hasi yasiyoweza kukadiriwa".
Chama hicho cha upinzani cha Cyprus Kusini kimesisitiza kwa kusema: "katika muktadha huu, mkusanyiko unaoendelea wa vikosi vya jeshi la Marekani kwenye kisiwa chetu, ndani na nje ya kambi za Uingereza, unaongeza hatari na wasiwasi".
Huku taarifa ya AKEL ikisisitiza kwamba, kwa mtazamo wa chama hicho Cyprus Kusini si ya kufanywa kituo cha majeshi ya kigeni bali ni ya kuwa daraja la amani na la kupitishia misaada ya kibinadamu, imeitaka serikali ya Ugiriki ya huko Cyprus ichukue hatua kwa kufuata mwelekeo huo.../