Borrell: EU iwawekee vikwazo mawaziri wawili wa Israel wenye misimamo mikali ya chuki
Aug 12, 2024 11:10 UTC
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameutaka umoja huo uwawekee vikwazo mawaziri wawili wenye misimamo mikali ya chuki wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Zaidi ya miezi tisa imepita tangu utawala wa Kizayuni uvamie Ukanda wa Ghaza kwa uungaji mkono kamili wa kijeshi na kidiplomasia wa Marekani; na katika muda wote huo, utawala huo haramu umefanya mauaji ya kimbari na jinai mbalimbali za kivita dhidi ya watu wasio na ulinzi wa eneo hilo bila kujali wala kuhofu mjibizo wowote wa jamii ya kimataifa.
Ukatili wa viongozi wahalifu wa Israel umekwenda mbali mpaka kufika hadi ya kuamsha sauti za shakhsia wahafidhina wa Magharibi ambao kwa kawaida huwa wanatosheka kueleza masikitiko yao tu kwa jinai zinazofanywa na utawala huo katili wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Kuhusiana na hilo na kwa mujibu wa IRNA, Josep Borrell ameandika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba: wakati dunia inashinikiza kusitishwa mapigano huko Ghaza, Itamar Ben-Gvir ametoa wito wa kupunguzwa upelekaji mafuta na misaada kwa raia huko Ghaza.
Mkuu huyo wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kwa kusema: vikwazo vinapasa viwe katika ajenda ya kufanyiwa kazi na Umoja wa Ulaya.
Aidha, Borrell ameongezea kwa kusema: ninaitaka Israel ijitenge waziwazi na uchochezi huu wa ufanyaji uhalifu wa kivita na kuonyesha nia njema kwa kushiriki katika mazungumzo ya kusitisha mapigano haraka.
Kabla ya hapo, mkuu huyo wa sera za nje wa EU alisema: kuwatesa kwa njaa makusudia raia ni uhalifu wa kivita, na kauli ya Smotrich ni dharau kwa sheria za kimataifa na kanuni za kimsingi za kibinadamu.
Itakumbukwa kuwa, waziri wa fedha wa utawala wa Kizayuni Bezalel Smotrich alitamka siku chache zilizopita kwamba hakuna anayetaka raia milioni mbili wa Ghaza wauawe au wafe kwa njaa, lakini jambo hilo linaweza kuwa ni la haki na la kimaadili mpaka mateka wa Israel watakaporejeshwa.../