Aug 12, 2024 11:56 UTC
  • Keir Starmer
    Keir Starmer

Keir Starmer Waziri Mkuu wa Uingereza ameshindwa kukamilisha mapumziko ya mwishoni mwa wiki na kurejea katika jengo nambari 10 huko Downing Street kufuatia vurugu na ghasia zinazoendelea kufanywa na wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali.

Starmer hadi sasa ameitisha vikao vitatu vya dharura kwa lengo la kudhibiti ghasia hizo. Karibu polisi elfu sita wametawanywa katika mitaa ya miji mbalimbali ya Uingereza ili kuzuia mashambulizi zaidi dhidi ya jamii ya Waislamu na wahajiri nchini humo. Baraza la wakuu wa polisi ya taifa ya Uingereza limeripoti kuwa, watu 779 wametiwa nguvuni, 349 miongoni wakituhumiwa kuhusika na machafuko hayo makubwa huko Uingereza. Machafuko na ukosefu wa usalama unaendelea kushuhudiwa katika aghalabu ya miji ya Uingereza licha ya kuimarishwa hatua kali za kiusalama. Televisheni ya Sky News imemnukuu Chris Hopkins mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kituo cha Utafiti cha Savanta na kuripoti kuwa: "Kwa kuzingatia ghasia na uvunjaji sheria ulioiathiri Uingereza, ungaji mkono wa wananchi kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo umepungua pakubwa tangu baada ya uchaguzi wa bunge. Sasa tunapasa kusubiri na kuona iwapo jibu la Keir Starmer kwa ghasia na machafuko hayo litakuwa na taathira za muda mrefu kwa misimamo na nafasi yake baina y wapiga kura wa nchi hiyo au la." 

Machafuko ya wafuasi wa mrengo wa kulia nchini Uingereza 

Taasisi ya YouGov imechapisha utafiti unaoonyesha kuwa nusu ya jamii ya watu nchini Uingereza wanaamini kuwa Starmer amefanya vibaya sana katika kukabiliana na machafuko makubwa yanayoikumba nchi yake. 

Ghasia kubwa zilianza katika aghalabu ya miji ya Uingereza mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, baada ya barobaro mmoja mwenye umri wa miaka 17 kushambulia hafla iliyokuwa ikifanyika katika shule moja ya watoto katika mji wa Southport. Watoto watatu waliuawa katika hujuma hiyo. Watoto wengine kadhaa na watu wazima wawili waliokuwa wamejeuhiwa vibaya, walipelekwa hospitali kufuatia shambulio hilo la kisu. Mara tu baada ya tukio hilo, habari za uongo zilichapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza kwamba barobaro huyo alikuwa mhajiri Mwislamu. Wafuasi wenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia walitumia vibaya taarifa hiyo ya uongo kama kisingizio cha kuanza kuwashambulia Waislamu, vituo na maneo yao ya ibada. 

Zaidi ya wiki moja sasa ambapo Waislamu wanakwenda kazini na majumbani mwao wakiwa wamejawa hofu na wasiwasi. Hata Waislamu mashuhuri wa Uingereza kama vile Humza Yousaf, aliyekuwa Waziri wa Kiongozi wa Scotland na Sadiq Khan, Meya wa London, hawafichi hofu na wasiwasi wao kutokana na machafuko hayo yanayowalenga Waislamu na wahajiri. Alipoulizwa kama anajisikia salama kama mwanasiasa Muislamu, Sadiq Khan amesema: "Ni wazi kuwa, sipo salama, ndiyo maana ninaishi chini ya ulinzi wa polisi wa saa 24." Tangu achaguliwa kuwa Meya mwaka wa 2016, Khan amepokea vitisho vingi na amesema: Timu ya polisi ya watu15 ina jukumu la kumlinda yeye na familia yake. 

Sadiq Khan, Meya wa jiji la London 

Mkewe, Saadia Ahmed, wakili mwenye asili ya Pakistani, pamoja na binti zao Anisah na Ammarah, wanalindwa na polisi. Humza Haroon Yousaf aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Scotland amesema kuwa kwa kuzingatia ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza yeye na familia yake huwenda wakalazimika kuondoka nchini humo kwa kuhofia ghasia na mashambulizi ya wafuasi wa mrengo wa kushoto wenye misimamo mikali. 

Waziri Kiongozi wa zamani wa Scotland ameongeza kuwa: Matamshi dhidi ya Uislamu na wahamiaji limekuwa jambo la kawaida nchini Uingereza; na sasa "yamedhihirishwa  kwa njia ya kutisha na ukatili zaidi." Wakati Waislamu mashuhuri nchini Uingereza wanapoeleza hofu na wasiwasi wao kuhusu maisha yao nchini humo, hali inaonekana kuwa ngumu zaidi na ya hofu kubwa kwa Waislamu walio wachache, hasa wahamiaji na wahajiri.