WHO: Wanaoambukizwa zaidi Mpox ni wanaume kupitia ngono
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa, kesi 9 kati ya 10 za homa ya nyani (Mpox) zinawakabili wanaume, ambapo aghalabu yao wanaambukizwa kwa njia ya zinaa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani, kesi 87,189 kati ya 90,410 zilizoripotiwa ni miongoni mwa wanaume, ambapo asilimia 96 kati yao waliambukizwa kupitia ngono.
Aidha ripoti hiyo ya WHO imeonyesha kuwa, virusi hivyo viliripotiwa miongoni mwa wanaume wenye umri wa kati ya miaka 29 na 41. Ripoti ya miripuko ya Mpox katika nchi nyingi ilikusanya data za maambukizi kutoka kwa mamlaka za kitaifa, kufikia Juni 30, 2024.
Jana Jumatano, Shirika la Afya Duniani liliitangaza Mpox kuwa "dharura ya afya ya umma" kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kabla ya hapo pia, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika CDC kilitangaza "dharura ya afya ya umma", kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, juu ya mripuko wa Mpox unaoenea kwa kasi katika bara hilo, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha kusambaa kwake.
Jumla ya visa 38,465 vya ugonjwa huo, ambao zamani ulijulikana kama homa ya nyani, vimerekodiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mwezi Januari 2022, pamoja na vifo 1,456, na ongezeko la 160% la kesi mwaka huu 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kulingana na data zilizochapishwa wiki iliyopita na Africa CDC.
Kesi za Mpox ziliripotiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita katika nchi za Burundi na Rwanda baada ya kuripoti mripuko wa maradhi hayo DRC; huku kesi zaidi zikigunduliwa pia nchini Kenya na Jamhuri ya Afrika ya Kati.