Marekani: Tunatamani Iran isiishambulie kijeshi Israel
-
John F. Kirby
Mratibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya Marekani, White House amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado ina nia ya kujibu mashambulizi na kuutia adabu utawala wa Kizayuni kwa kuupiga kwa silaha lakini amesema kuwa, anatamani Iran isifanye hivyo.
John F. Kirby amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya CNN ya Marekani yaliyorushwa hewani jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa ilizo nazo Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado imekusudia kuishambulia kijeshi Israel.
Amesema, hata wao katika Ikulu ya White House wanaamini hivyo hivyo kwamba Iran itaipiga Israel katika siku zijazo, lakini tunatamani shambulio hilo lisifanyike.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya ujuba wa kumshambulia na kumuua kigaidi Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniyeh wakati alipokuwa mgeni rasmi wa Iran hapa Tehran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado inatangaza nia yake ya kujibu ujuba huo kwa kuutia adabu utawala pandikizi wa Kizayuni katika muda, mahala na wakati itakaoamua Tehran kwani hiyo ni haki yake ya wazi kabisa ambayo hakuna yeyote anayeweza kuipinga duniani.
Tangu wakati huo madola mbalimbali hasa ya Magharibi yamekuwa yakiibembeleza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isiitie adabu Israel. Wajumbe pamoja na mawasiliano mbalimbali yakiwemo ya moja kwa moja ya simu baina ya Iran na wakuu wa nchi za Ulaya na Marekani yamekuwa yakifanyika takbiran kila siku kujaribu kuiombea Israel isipigwe, lakini Iran bado imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuutia adabu utawala wa Kizayuni.