Mpox yafika Ulaya baada ya kuua mamia barani Afrika
Baada ya kuua mamia ya watu barani Afrika, sasa umonjwa wa Mpox umeripotiwa kuingia barani Ulaya hususan Sweden.
Ni baada ya Sweden kutangaza kisa cha kwanza cha ugonjwa huo ambao umeua watu 548 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni ishara ya kuenea kwake nje ya bara la Afrika.
Shirika la Afya ya Umma la Uswidi lilithibitisha jana Alhamisi kwamba aina ya Mpox imegunduliwa kwa mgonjwa katika mji mkuu wa nchi hiyo.
Mtaalamu wa magonjwa Magnus Gisslen amesema mtu huyo aliyepatikana na Mpox alitembelea "Afrika ambako kuna mlipuko mkubwa wa Mpox clade I."
Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatano iliyopita lilitangaza mlipuko wa Mpox nchini DRC na nchi nyingine za Afrika kama "dharura ya afya duniani".
Wakati huo huo, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika kimetangaza "dharura ya afya ya umma", kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, kuhusu mlipuko wa Mpox unaokua katika bara hilo, na kutoa "wito wa kuchukuliwa hatua" za kukomesha msambao wake.
Jumla ya visa 38,465 vya ugonjwa huu, ambao zamani ulijulikana kama Homa ya nyani, vimerekodiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mwezi Januari 2022, pamoja na vifo 1,456, na ongezeko la 160% la kesi mnamo mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kulingana na data zilizochapishwa wiki iliyopita na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, Africa CDC.
Kesi za Mpox ziliripotiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita katika nchi za Burundi na Rwanda, huku kesi zaidi zikigunduliwa pia nchini Kenya na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa, kesi 9 kati ya 10 za homa ya nyani (Mpox) zinawakabili wanaume, ambapo aghalabu yao wanaambukizwa kwa njia ya zinaa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani, kesi 87,189 kati ya 90,410 zilizoripotiwa ni miongoni mwa wanaume, ambapo asilimia 96 kati yao waliambukizwa kupitia ngono.