Mchango wa madola ya Magharibi katika machafuko ya Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115292-mchango_wa_madola_ya_magharibi_katika_machafuko_ya_asia_magharibi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Massoud Pezeshkian amesema kuwa, himaya na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni ndio sababu kuu na muhimu katika kuhatarisha usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 16, 2024 07:05 UTC
  • Mchango wa madola ya Magharibi katika machafuko ya Asia Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Massoud Pezeshkian amesema kuwa, himaya na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni ndio sababu kuu na muhimu katika kuhatarisha usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia.

Eneo la Asia Magharibi daima limekuwa lkitaabika kwa jinamizi la ukosefu wa usalama na machafuko. Ukosefu huu wa usalama na machafuko ulichukua wigo mpana zaidi kuanzia 2011. Uingiliaji wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani katika masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu ulikuwa ndio sababu ya kuzuka misimamo mikali na tatizo la ugaidi katika nchi hizo, na kilele cha uingiliaji huo kilitokea nchini Syria.

Kadhalika, uungaji mkono wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kwa vita vya utawala wa Saudi Arabia dhidi ya nchi masikini ya Yemen ndio chanzo cha maafa makubwa zaidi ya binadamu katika karne ya 21. Hata hivyo vita vya Gaza ni uwanja wa kilele cha uungaji mkono wa Wamagharibi unaoongozwa na Marekani kwa jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza.

Katika miaka 76 iliyopita, utawala wa Kizayuni daima umekuwa ukitenda jinai dhidi ya wananchi wa Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza, lakini vita vya hivi karibuni na mauaji ya halaiki ya hivi sasa kwa hakika hayana mfano. Katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, utawala wa Kizayuni umeua zaidi ya Wapalestina 40,000 na kujeruhi zaidi ya watu elfu 93. Wengi wa mashahidi na waliojeruhiwa huko Gaza ni wanawake na watoto.

Raus wa Iran (kushoto) na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer

 

Fauka ya hayo, Wazayuni wamefanya jinai kubwa kwa kushambulia makazi ya rai, vituo vya matibabu, hospitali, shule na maeneo ya ibada. Hata hivyo madola ya Magharibi ambayo daima yamekuwa yakipigia kelele haki za binadamu, yakiongozwa na Marekani yaliunga mkono jinai za Wazayuni na kudai kuwa eti: "Unachofanya utawala wa Kizayuni kinachukuliwa kuwa ni kujilinda." Hivi kushambulia kwa mabomu misikiti, shule, vituo vya afya na hospitali ni kujilinda? Kuua wagonjwa na watoto wadogo wasio na hatia kunahesabiwa kuwa ni kujilinda?

Mbali na uungaji mkono wa kisiasa na kidiplomasia, madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, pia yametoa uungaji mkono mkubwa wa kiuchumi na kijeshi kwa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi 11 iliyopita. Msaada huo wa kiuchumi umetolewa ili kuhakikisha kwamba baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu halikabiliwi na changamoto za kiuchumi na za ndani katika kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.

Uungaji mkono huo wa kijeshi pia unafanywa kwa ajili ya:

Mosi, utawala wa Kizayuni uendeleze mauaji ya halaiki huko Gaza kwa urahisi na bila wasiwasi, na pili hofu na wasiwasi wa utawala wa Kizayuni kuhusu hatua za Iran na makundi ya muqawama upungue.

Wapalestina wasiopungua 40,000 wameuawa shahidi na Isarel tangu Oktoba mwaka jana (2023)

 

Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ulitekeleza jinai ya  kumuua hapa mjini Tehran Ismail Haniyeh, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, umekabiliwa tishio kali la kuitishia Jamhuri ya Kiislamu na kuufanya uingiwe na kiwewe.

Kuhusiana na suala hilo, serikali ya Marekani imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kiwango ambacho hakina mithili ili kutuma ujumbe wa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni. Jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na vile vile kitendo cha  jinai dhidi ya ardhi na mamlaka ya kujitawala Iran ni sababu muhimu katika kutishia usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia.

Uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani kwa jinai za Wazayuni umekuwa na nafasi na mchango muhimu katika kuhatarisha usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kwa hakika nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ndizo chanzo kikuu cha ukatili wa Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza na tishio la usalama wa eneo hilo.

Ni kwa muktadha huo, ndio maana Rais Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akasema katika mazungumzo yake ya simu na Keir Starmer, Waziri Mkuu wa Uingereza kwamba, kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni na ambazo hazijawahi kurekodiwa katika historia huko Gaza, pamoja na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Magharibi kwa utawala huo dhalimu, ni mambo ambayo yanakwenda kinyume na sheia za kimataifa na yanachochea jinai zaidi kama ambavyo pia yanahatarisha usalama wa eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.