Hali ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya waliofanyiwa ukatili mkubwa Myanmar bado ni mbaya
Hali mbaya ya Waislamu wa Rohingya, kabila la walio wachache kutoka Jimbo la Rakhine nchini Myanmar, inaendelea kuwa mbaya na kuliza walimwengu wenye hisia za kibinadamu huku kukiwa hakuna matumaini ya Waislamu hao kurejea kama walivyokuwa kabla ya kufanyiwa ukatili wa kutisha na mabudha na wanajeshi wa Myanmar.
Ripoti za hivi karibuni kabisa za mashirika ya misaada zinasema kuwa katika kipindi cha miaka saba iliyopita, zaidi ya watu milioni 1.3 wa jamii ya Waislamu wa Rohingya walioporwa makazi yao na kulazimishwa kukimbia kwa nguvu, wamekuwa wakihangaika na kuishi katika mazingira magumu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba: "Mwishoni mwa mwaka wa 2023, takriban watu milioni 117.3 kote duniani walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na mateso, migogoro, ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu n.k."
Miongoni mwa wakimbizi hao ni Warohingya milioni 1.3 ambao wengi wao ni Waislamu wenyeji wa Myanmar. Mara nyingi jamii ya Warohingya inatajwa kwa jina la jamii ya wachache wanaoteswa zaidi duniani. Wengi wao hivi sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi zenye msongamano mkubwa wa watu katika wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh.
Licha ya kuongezeka misaada kutoka kwa mashirika ya kibinadamu, lakini bado misaada ya kigeni inahitajika zaidi kutokana na hali mbaya wanayoishi wakimbizi hao ambao hawawezi tena kurejea kwenye nchi na maeneo yao ya jadi katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar, kutokana na ukatili mkubwa wa wanajeshi na mabudha wenye misimamo mikali.