Chuki dhidi ya Uislamu zaongezeka nchini Ufaransa
Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka nchini Ufaransa na mara hii ni katika mji wa Lyon.
Gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limeandika, kuta za msikiti mmoja wa eneo la Bron katika mji wa Lyon, jana (Jumatano) iliandikwa maneno ya kibaguzi na vitisho dhidi ya Waislamu.
Baadhi ya maandishi hayo yamesema kuwa, Waislamu wote watauawa na kumalizwa nchini Ufaransa kama hawataondoka nchini humo.
Belqacim Louhichi, mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni ya Waislamu (ACMB) amethibitisha habari hiyo ya kuendelea kuvunjiwa heshima misikiti ya eneo hilo na amesema kuwa, watafungua mashtaka mahakamani kulalamikia jambo hilo.
Kwa upande wake, Michel Delpuech, mmoja wa wakuu wa manispaa ya mji wa Lyon amelaani kitendo cha maadui hao wa Uislamu na kusema kuwa, kinalenga kuleta mifarakano na kuhatarisha umoja wa kitaifa nchini Ufaransa.
Vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika miezi ya Januari na Novemba 2015 pamoja na yale ya mwezi Julai 2016 nchini Ufaransa.
Mara kwa mara Waislamu wa Ufaransa wamekuwa wakilaani mashambulio hayo na kusisitiza kuwa, hayana uhusiano wowote wa dini tukufu ya Kiislamu.