100 wapoteza maisha kutokana na mafuriko China
https://parstoday.ir/sw/news/world-i11701-100_wapoteza_maisha_kutokana_na_mafuriko_china
Watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kaskazini mwa China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2016 09:46 UTC
  • 100 wapoteza maisha kutokana na mafuriko China

Watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kaskazini mwa China.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, watu 24 wamethibitishwa kuaga dunia kutokana na janga hilo la kimaumbile katika mkoa wa Hebei, kaskazini mwa nchi. Aidha zaidi ya watu 70 wanahofiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo katika mikoa ya Shanxi, Henan na Shaanxi. Zaidi ya watu 123,000 wamelazimika kuyahama makazi yao katika miji 11 ya mkoa wa Hebei kutokana na mafuriko hayo yaliyosomba nyumba zaidi ya 7000. Mbali na vifo na kusombwa makazi ya watu, mafuriko hayo vilevile yamekata njia za mawasiliano na kuathiri sekta ya uchukuzi.

Timu ya uokozi China ikisaidia kuwavusha baadhi ya raia waliokwama baada ya mafuriko

Mapema mwezi huu, watu 112 walipoteza maisha kutokana na mafuriko na vimbunga vilivyosababishwa na mvua kubwa katikati na kusini mwa China. Itakumbukwa kuwa, zaidi ya watu 4,000 walifariki dunia kutokana na mafuriko katika eneo la Yangtze nchini China mwaka 1998.