Russia yataka BRICS iunde mbadala wa IMF
(last modified 2024-10-11T10:32:55+00:00 )
Oct 11, 2024 10:32 UTC
  • Russia yataka BRICS iunde mbadala wa IMF

Russia ambayo ni mwenyekiti wa kiduru wa kundi la BRICS mwaka huu, imetoa wito kwa washirika wake kubuni njia mbadala ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kukabiliana na shinikizo la kisiasa kutoka mataifa ya magharibi kabla ya mkutano wa kilele wa BRICS baadaye mwezi huu.

Mwito huo umetolewa katika mkutano wa maafisa wa ngazi za juu wa masuala ya fedha na benki kuu za nchi wanachama wa BRICS huko Moscow, mji mkuu wa Russia.

Waziri wa Fedha wa Russia, Anton Siluanov ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, amesema nchi za Magharibi zinadhibiti mfumo wa kifedha wa kimataifa na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuundwa mfumo mbadala.

Waziri Siluanov ameeleza bayana kuwa, "IMF na Benki ya Dunia hazitekelezi majukumu yao (ipasavyo). Hazifanyi kazi kwa maslahi ya nchi za wananchama wa BRICS." 

BRICS ilianzishwa mwaka 2006 na awali ilijumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Wanachama wapya wa jumuiya hiyo ni pamoja na Iran, Misri, Ethiopia, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Nchi nyingi zikiwemo za Afrika zimetuma maombi ya kujiunga na jumuiya hiyo.

Jumuiya hiyo, ambayo inaonekana zaidi kama mbadala wa kiuchumi na kisiasa wa kukabiliana na ukiritimba wa Magharibi, inaunda karibu asilimia 46 ya watu wote duniani, asilimia 36 ya pato ghafi la taifa (GDP), na asilimia 25 ya biashara ya kimataifa inayopimwa kwa misingi ya mauzo ya nje.

Tags