Kuundika mwafaka wa kimataifa dhidi ya Israel
Utawala wa Kizayuni unaendelea kulaaniwa na kukosolewa pakubwa kimataifa kufuatia kuendelea jinai kubwa za utawala huo katika vita vya Gaza hususan mauaji ya kimbari unayotekekeleza dhidi ya Wapalestina na hivi sasa mashambulizi ya kila upande dhidi ya Lebanon ambayo yamewaua shahidi maelfu ya watu na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine huko Gaza na Lebanon.
Aidha hivi sasa kumeundika mwafaka wa kimataifa dhidi ya Israel ambao umeutenga pakubwa utawala huo katika sura mbalimbali.
Moja ya madhihirisho ya kuasisiwa mwafaka dhidi ya utawala wa Kizayuni ni upinzani wa nchi nyingi dhidi ya misimamo na hatua za utawala huo dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kuhusiana na suala hilo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimesaini barua zikimuunga mkono katibu mkuu huyo na kuukosoa utawala wa Kizayuni kwa kitendo chake cha kumpiga marufuku Antonio Guterres kusafiri katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na kumwita kuwa mtu asiyetakikana huko.
Nchi 105 wanachama wa UN zimesaini barua hiyo katika kuonyesha uungaji mkono wao mkubwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Nchi hizo zimebainisha wasiwasi wao mkubwa na kulaani uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni wa kumpiga marufuku Guterres kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Barua hiyo inasema: 'Vitendo hivyo vinadhoofisha uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kutekeleza majukumu yake, ambayo ni pamoja na kusuluhisha migogoro na kuwasilisha misaada ya kibinadamu.' Nchi zilizosaini barua hiyo zimeongeza kuwa: "Tunathibitisha kumuunga mkono kikamilifu na kumuamini Katibu Mkuu na utendaji wake. Tukiwa kama nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tunataka kuheshimiwa kiongozi wa Umoja wa Mataifa na majukumu yake."
Shaksia asiyetakiwa au kukaribishwa (Persona non grata) ni neno katika sheria za kimataifa ambalo linaweza kutumiwa na serikali kuhusu raia wa serikali nyingine, hasa wanadiplomasia. Mtu ambaye anafahamika kama shaksia asiyekaribishwa hana haki ya kuingia au kuwepo katika nchi mwenyeji.
Msimamo huu wa Israel dhidi ya Antonio Guterres unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni unauheshimu tu Umoja wa Mataifa na maafisa wake wa ngazi ya juu wakati wanapoakwenda sambamba na maslahi na malengo yake lakini pale wanapokwenda kinyume kidogo tu na matakwa ya viongozi wa utawala wa Kizayuni, hukabiliwa na radiamali kali na kutajwa kuwa ni "shaksia wasiotakikana" na kuzuiwa kuingia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Israel Katz siku kadhaa ziliopita alimpiga marufuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kumwita kuwa mtu asiyekaribishwa. Nchi mbalimbali duniani zimekosoa uamuzi huo na kusema kuwa unakinzana na jitihada za kurejesha amani katika eneo la Mashariki ya Kati. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alidai kuwa yeyote ambaye hawezi kulaani waziwazi oparesheni ya makombora ya Iran dhidi ya Israel hastahili kukanyaga Israel yaani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hii si mara ya kwanza kwa Israel kumshambulia kwa maneno makali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Kizayuni huko nyuma alimtaka Katibu Mkuu wa UN ajiuzulu katika radiamali yake kwa matamshi ya Guterres kuhusu chanzo cha oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na rekodi mbovu ya jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.
Bila shaka, misimamo iliyodhihirishwa na nchi mbalimbali dhidi ya Israel kutokana na jinai na hatua zake zilizo kinyume cha sasa imeenea pia katika nyuga nyingine. Miongoni mwa kadhia muhimu za hivi karibuni katika uwanja huu ni kulaaniwa Israel kufuatia shambulio lake la makusudi dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNIFIL) na ombi la nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Ulaya la kutaka kusimamishwa mashambulizi hayo. Kadiri kwamba hata Marekani imetaka kukomeshwa mashambulizi hayo na kutokaririwa tena. Vikosi vya UNIFIL vimetumwa katika maeneo ya mpaka wa kusini mwa Lebanon na kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa. Juzi Alhamisi askari jeshi wawili wa kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa walijeruhiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na Ijumaa pia wanajeshi wengine wawili walijeruhiwa. Msemaji mmoja wa UNIFIL ameviambia vyombo vya habari kuwa Israel imetekeleza mashambulizi hayo kwa makusudi.
Kuhusiana na suala hilo, nchi tatu za Ulaya, Ufaransa, Italia na Uhispania katika taarifa yao ya pamoja zimetaja mashambulizi hayo ya makusudi kuwa ni jambo lisilokubalika na kutaka kusitishwa mara moja. Taarifa hiyo imesema kuwa hatua ya Israel ya kuvishambulia vikosi vya UNIFIL ni ukiukaji wa wazi wa azimio la kimataifa nambari 1701 lililopasishwa na Baraza la Usalama. Wakati huo huo, viongozi wa nchi za Magharibi wamelaani vikali mashambulizi hayo ya Israel, huku wakiwa wamenyamazia kimya jinai na mashambulizi ya kinyama ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya raia wa Gaza na Lebanon. Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amelitaja shambulio la Israel dhidi ya vikosi vya UNIFIL kusini mwa Lebanon kuwa halikubaliki na akauonya utawala huo kutowagusa wanajeshi wa Italia. Amesisitiza kuwa kuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa wanajeshi wa Israel wamehusika na shambulio hilo katika vituo vya UNIFIL. Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Ulaya amelaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na kuyataja kuwa hayakubaliki. Viongozi wa nchi za Ufaransa na Italia pia wamewasilisha ombi wakitaka kuitishwa kikao baina ya nchi zilizotuma wanajeshi wake katika kikosi cha UNIFIL. Wakati huo huo Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa Israel nayo imelazimika kuchukua msimamo kuhusu kadhia hii. Rais Joe Biden wa nchi hiyo amesema kuwa anaitaka Israel iache kuwashambulia askari jeshi wa UNIFIL huko Lebanon.
Licha ya takwa hili lililowasilishwa na washirika na waitifaki wa Magharibi wa Tel Aviv lakini utawala wa Kizayuni hautilii maanani kivyovyote ombi hilo, na unaendelea na vitendo vyake vya jinai dhidi ya binadamu. Kushambuliwa hospitali ya Taasisi ya Hilali Nyekundu ya Iran katika mpaka wa Syria na Lebanon ni miongoni mwa hujuma mpya za utawala wa Kizayuni. Kitendo hiki cha utawala ghasibu wa Israel ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za haki za kibinadamu ambazo zinapiga marufuku kushambuliwa vituo vya matibabu na misaada ya kibinadamu.