Mtikisiko wa kiuchumi US; Boeing kuwatimua wafanyakazi 17,000
(last modified Sun, 13 Oct 2024 02:14:07 GMT )
Oct 13, 2024 02:14 UTC
  • Mtikisiko wa kiuchumi US; Boeing kuwatimua wafanyakazi 17,000

Kampuni ya Boeing inayoongoza nchini Marekani kutengeneza ndege za kibiashara na kijeshi imetangaza mpango wake wa kuwapiga kalamu nyekundu wafanyakazi 17,000 wa shirika hilo; huku mgomo wa wafanyakazi 33,000 wa kampuni hiyo huko West Coast ukitokota.

Kelly Ortberg, Rais na Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa Boeing amesema katika taarifa kuwa, "Tunaangalia upya idadi ya wafanyakazi wetu ili kuendana na uhalisia wetu wa kifedha, na kuangalia zaidi vipaumbele vyetu."

Ortberg ameongeza kuwa, "Katika miezi ijayo, tunapanga kupunguza idadi kubwa ya wafanyakazi wetu kwa takriban asilimia 10. Mapunguzo haya yatajumuisha watendaji, wakurugenzi na wafanyakazi."

Mvutano kuhusu mishahara ulisimamisha mazungumzo baina ya kampuni hiyo na wafanyakazi hao, na hivyo kupelekea wafanyakazi hao kugoma.

Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2019, nchi kadhaa duniani zilipiga marufuku ndege ya Kimarekani aina ya Boeing 737 Max kufuatia kuanguka ndege mpya ya aina hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia huko Addis Ababa, ambapo abiria na wahudumu wote 157 waliokuwamo walipoteza maisha.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Arlington ya US pia ameonya na kuwataka wawekezaji na wanahisa wa shirika hilo kujitayarisha kwa hasara "kubwa" inayojongea. Amewaasa wanahisa wa kampuni hiyo kujiandaa kwa vita virefu na wafanyakazi.