Uingereza yakiri kuwa Saudia inatenda jinai za kutisha Yemen
Katika hatua isiyo ya kawaida na ambayo haikutarajiwa na wengi, Uingereza imekiri kuwa yumkini muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika hujuma za anga dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen umekiuka sheria za kibinadamu.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa, mashambulizi ya anga ya muungano wa kijeshi nchini Yemen katika miezi ya hivi karibuni yamekiuka sheria za kimataifa. Msimamo huu mpya wa serikali ya London umekuja mwezi mmoja baada ya Umoja wa Mataifa kutoa ripoti iliyoonyesha kuwa, watoto zaidi ya 500 wameuawa katika hujuma za anga za muungano huo vamizi nchini Yemen.
Itakumbukwa kuwa, Saudia iliunda muungano wa kichokozi kwa kuzishirikisha baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Imarati kwa uungaji mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuanzisha mashambulizi makali ya anga mwezi Machi mwaka 2015 dhidi ya watu wa Yemen, ambayo yaliandamana na mzingiro wa kila upande dhidi ya nchi hiyo.
Hata hivyo licha ya Riyadh na waitifaki wake kutekeleza hujuma hizo kubwa zilizokuwa na lengo la kutaka kumrejesha madarakani rais aliyejiuzulu wa nchi hiyo, Abd Rabbuh Mansur Hadi, bado hujuma hizo hazijazaa matunda na badala yake zimeishia kufeli mbali na kusababisha maafa makubwa dhidi ya maelfu ya watu wa Yemen wakiwemo watoto, wanawake na raia wa wakawaida wa nchi hiyo. Wayemen zaidi ya 10,000 wameripotiwa kuuawa katika hujuma hizo kufikia sasa.
Wiki iliyopita, harakati ya Ansarullah ilianza mazungumzo na kundi linaloungwa mkono na Saudi Arabia la Abdu Rabbuh Mansru Hadi nchini Kuwait, baada ya mazungumzo hayo kukwama kwa muda wa wiki mbili.
Hata hivyo, mkuu wa timu ya harakati ya Ansarullah katika mazungumzo hayo, Muhammed Abdulsalam alisema jana kuwa, mazungumzo hayo ya Kuwait ni ya kupoteza muda, kwani muhusika mkuu wa uvamizi wa Yemen, yaani Saudi Arabia, hashiriki moja kwa moja.