UNESCO: Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku 4 duniani kote
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetoa ripoti yake ya kila mwaka leo Jumamosi, kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Uhalifu unaofanywa dhidi ya Waandishi wa Habari, likimulika zaidi ongezeko la idadi ya waandishi wa habari waliopoteza maisha wakitekeleza wajibu wao katika miaka ya hivi karibuni.
Takwimu za UNESCO zinaonyesha kuwa, mwanahabari mmoja ameuawa kila baada ya siku 4 duniani kote katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, kiwango cha mauaji ya waandishi wa habari kimeongezeka kwa takriban 38% ikilinganishwa na ripoti ya awali, jambo ambalo linaashiria kushuka kwa kiwango kikubwa usalama wa waandishi wa habari. Kulingana na ripoti hiyo, kesi 162 zilizothibitishwa za mauaji ya waandishi wa habari zilirekodiwa mwaka 2022 na 2023, na kwamba zaidi ya nusu yao walikuwa katika nchi zinazokumbwa na mizozo ya kivita.
Ardhi ya Palestina imeongoza orodha ya nchi hatari zaidi kwa maisha ya waandishi wa habari katika 2023, huku Mexico ikishuhudia kiwango cha juu zaidi mnamo 2022, ikirekodi mauaji 19 ya waandishi habari. Amerika ya Kusini na Karibi na nchi za Kiarabu, ni maeneo ambako idadi kubwa ya waandishi wa habari wameuawa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, waandishi wengi wa habari waliopoteza maisha katika nchi ambazo hazikushuhudia mizozo ya moja kwa moja waliuawa walipokuwa wakifuatilia masuala ya uhalifu uliopangwa na ufisadi, au walipokuwa wakiandika habari za maandamano, suala ambalo linaakisi hatari kubwa inayowaandama wafanyakazi wa vyombo vya habari.
Mgogoro wa mauaji ya waandishi wa habari hasa katika Ukanda wa Gaza ambako Israel inaendelea kufanya mauaji ya kimbari, ulitawala Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari la Umoja wa Mataifa kuhusu Amani Mashariki ya Kati mwaka 2024, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alidokeza kuwa idadi ya waandishi habari waliouawa Gaza imefikia "kiwango kisicho na kifani."
Guterres alitoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kulinda wanataaluma wa vyombo vya habari na kuhakikisha kwamba waliohusika wanawajibishwa.