Jerusalem Post: Jeshi la Israel linamshinikiza Netanyahu asitishe vita, hasara zimezidi
Gazeti la Jerusalem Post limeripoti kuwa taasisi ya kijeshi ya Israel inataka kusitishwa vita katika maeneo ya Gaza na Lebanon, kwa sababu inaamini kuwa hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana kijeshi.
Gazeti hilo limefichua katika ripoti ya mwandishi wake mkuu wa masuala ya kijeshi na mchambuzi wa masuala ya kijasusi, Yonah Jeremy Bob, kwamba jeshi la Israel limechanganyikiwa kutokana na hasara ya kila siku miongoni mwa wanajeshi wake.
Jeremy Bob amedokeza kwamba Mkuu wa Jeshi la Israel, Herzi Halevy na Waziri wa Ulinzi, Yoav Galant wamezidisha mashinikizo kwa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, ili kufikia usitishaji wa mapigano huko Gaza ambao utarudisha nyumbani wafungwa 101 walio hai wa Israel na maiti za waliosalia zilizoko mikononi mwa Harakati za Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).
Ijumaa ya jana pia, gazeti la Yedioth Ahronoth liliripoti kwamba mwezi uliomalizika majuzi wa Oktoba ndio ulikuwa wa "umwagikaji damu zaidi" tangu Oktoba 7, 2023, kwa sababu Waisraeli 88 wameuawa katika mwezi huo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, wanajeshi 37 wa Israel waliuawa katika makabiliano na wapiganaji wa Hizbullah kusini mwa Lebanon na kwenye mpaka wa kaskazini, huku wengine 19 wakiuawa katika Ukanda wa Gaza.
Kwa upande mwingine, harakati ya Hizbullah ilitangaza - Alhamisi iliyopita- kwamba zaidi ya wanajeshi na maafisa 95 wa Israel wameuawa na wengine wapatao 900 kujeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon mnamo Septemba 30 mwaka jana.
Taarifa ya Hizbullah ilieleza kuwa wapiganaji wake wameharibu vifaru 42 vya Merkava, tingatinga 4 za kijeshi, magari mawili aina ya Hummer, gari la kivita na shehena ya kubebea wanajeshi, pamoja na kuangusha ndege 5 zisizo na rubani za Israel.